Israel kuendeleza vita baada ya kusitishwa

Muktasari:
- Serikali ya Israel imesema mapigano yataendelea hata baada ya kumalizika muda unaopendekezwa wa kusitisha mapigano na kubadilishana mateka kati yake na wanamgambo wa Hamas.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amesema kufikiwa kwa makubaliano ya usitishwaji wa mapigano, hakutafanya vita kati yake na wanamgambo wa Hamas kukoma.
“Jeshi la Israel litaendelea na mapambano baada ya kusitishwa kwa muda, tuko vitani, na tutaendeleza vita, tutaendelea hadi tutimize malengo yetu yote,” amesema Netanyahu.
Israel imeapa kuendeleza vita hadi itakapoharibu uwezo wa kijeshi wa Hamas na kuwarudisha mateka wote.
Leo Novemba 22, 2023; Shirika la Habari la LBC limeripoti kuwa Netanyahu ameitisha vikao vingi kuzungumzia suala la makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo hao.
Ripoti mbalimbali za vyombo vya habari vya Israel zimesema kwamba makubaliano hayo yatasababisha kusitishwa kwa mapigano kwa siku kadhaa kati ya Israel na Hamas.
Aidha makubaliano hayo yatawezesha mateka 50 kati ya 240 wanaoshikiliwa na Hamas kuachiwa huru, huku wafungwa 150 wa Kipalestina wanaoshikiliwa na Israel wataachiwa na kwamba shughuli hiyo inatarajiwa kufanyika Alhamisi au Ijumaa wiki hii.
Kwa upande mwingine, nchi ya Qatar ambayo ndiyo mpatanishi wa mzozo huo, imesema idadi ya wanawake na watoto wa Kipalestina wanaozuiliwa katika magereza ya Israel wataachiwa kwa kubadilishana na mateka.
Naye, Waziri wa zamani wa sheria wa Israel, Yossei Beilin ameiambia LBC kuwa makubaliano ya kuwaachilia mateka wa Israel ni ushindi kwa Hamas. Amesema kundi hilo linaamuru masharti na linaweza kusukuma vikosi vya Israeli kurudi nyuma.
Erdogan aitupia lawama Israel
Wakati huohuo Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan leo Jumatano amesema wanachokifanya Israel huko Gaza na maeneo mengine ya Palestina ni uhalifu dhidi ya ubinadamu, unaohusisha mauaji ya halaiki.
"Lazima tuilazimishe Israel kuzingatia sheria za kimataifa na kuwajibishwa kwa matendo yake. Tunapaswa pia kuvunja vikwazo katika Umoja wa Mataifa," Erdogan amenukuliwa na Shirikas la Anadolu Agency alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Ikumbukwe Israel ilianzisha mashambulizi ya anga na ardhini katika Ukanda wa Gaza saa chache baada ya shambulio la Oktoba 7 la Hamas, ambapo hadi sasa zaidi ya Wapalestina 14,128, wakiwemo watoto 5,840 na wanawake 3,920 wameuawa kulingana na mamlaka za afya katika eneo hilo. Idadi ya vifo vya Israeli ni zaidi ya 1,200, kulingana na takwimu rasmi.
Maelfu ya majengo, ikiwa ni pamoja na hospitali, misikiti na makanisa pia yameharibiwa katika mashambulizi ya anga na ardhini ya Israeli kwenye eneo lililozingirwa.
Imeandikwa na Sute Kamwelwe kwa msaada wa mashirika.