Mafuta yatajwa kizuizi cha misaada Gaza
Muktasari:
- Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi wa Kipalestina (Unrwa), Juliette Touma amesema ili waweze kutoa misaada katika ukanda wa Gaza, lita 120,000 za mafuta zinahitajika kila siku.
Gaza. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia wakimbizi wa Kipalestina (Unrwa), Juliette Touma amesema ili waweze kutoa misaada katika ukanda wa Gaza, lita 120,000 za mafuta zinahitajika kila siku.
DW imeripoti kuwa Touma amesema ukosefu wa nishati hiyo pamoja na kukatika kwa mawasiliano, kunaitatiza Unrwa kutoa misaada hiyo ya kibinadamu.
Touma amenukuliwa akisema kuwa mpaka jana, hapakuwa na mafuta yaliyofikishwa Gaza japo inadaiwa kuwa Baraza la Mawaziri la Israel linaloshughulika na vita hivyo, limeidhinisha malori mawili ya mafuta kuingia Gaza yakitokea Misri kila siku.
Kwa upande mwingine, kampuni za mawasiliano ya simu za Paltel na Jawwal zimesema kuwa huduma za simu na intaneti zimerejeshwa kwa sehemu katika Ukanda wa Gaza.
Taarifa zimesema hatua hiyo ilijiri baada ya kuingizwa kwa kiasi fulani cha mafuta kupitia shirika la Unrwa, Shirika la Habari la AFP liliripoti kuwa maofisa wa mpaka wa Gaza walisema lita 17,000 za mafuta zilifikishwa katika ukanda huo jana usiku.
Wizara ya Afya ya Gaza inayoongozwa na Hamas imesema kuwa idadi ya vifo katika ukanda huo kufuatia operesheni ya kijeshi ya Israel, inayoendelea tangu mashambulizi ya kigaidi ya Oktoba 7 imefikia watu 12,000.
Idadi hiyo ni Pamoja na karibu watoto 5,000 na wanawake 3,000. Wizara hiyo imesema watu wengine 30,000 wamejeruhiwa.
Awali, wizara hiyo ilisema isingeweza kutoa idadi kamili ya vifo kutokana na ugumu wa kuiondoa miili kutokana na mapigano makali.
Wanajeshi wa Israel waliendelea na msako wao kwa siku ya tatu jana Ijumaa katika hospitali ya Al-Shifa, wakitafuta kile wanachosema ni kituo cha kamandi ya Hamas ambacho makamanda wao wanasema kimefichwa katika mahandaki yaliyoko chini ya hospitali hiyo.
Wanamgambo hao na wakurugenzi wakuu wa hospitali hiyo wanakanusha kuwepo kwa kituo cha aina hiyo mahali hapo.
Mjini Berlin, katika kikao cha pamoja cha waandishi habari jana usiku, Kansela wa Ujerumani, Olaf Scholz alisisitiza kuwa haki ya Israel ya kujilinda haipaswi kutiliwa shaka.
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan wakati huo huo, aliendeleza ukosoaji wake mkali wa operesheni ya Israel inayoendelea Gaza akilaani kushambuliwa hospitali na kuwaua watoto.
Akizungumza na waandishi habari wakati wa ziara ya Erdogan mjini Berlin, Scholz amesema sio siri kuwa yeye na rais wa Uturuki wana mitazamo tofauti kabisa kuhusu mzozo huo wa sasa.
Scholz amesema hakuna nafasi ya chuki dhidi ya wayahudi nchini Ujerumani, bila kujali kama inachochewa kisiasa au kidini, kama inasababishwa na siasa za mrengo wa kulia au kushoto, kama imekulia Ujerumani kwa karne nyingi au inaingizwa nchini kutoka nje ya nchi.
Erdogan, ameongeza kuwa iwapo Ujerumani itaungana na Uturuki katika kutoa wito wa kusitishwa mapigano Gaza, kuna nafasi ya hilo kufanyika.