Israel yabadili Waziri wa Mambo ya Nje

Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Eli Cohen (kushoto), na kulia ni Waziri mpya wa Mambo ya nje, Israel Katz. Times of Israel

Muktasari:

  • Israel Katz sasa ndiye Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Israel akichukua nafasi ya Eli Cohen.

Dar es Salaam. Wakati mapambano yakiendelea kati ya Israel na kikundi cha Hamas cha Palestina, leo Serikali ya Israel imetangaza kuteua Waziri mpya wa Mambo ya Nje, Shirika la Habari la AFP limeripoti.

Israel Katz sasa ndiye Waziri mpya wa Mambo ya Nje wa Israel akichukua nafasi ya Eli Cohen.

Awali Katz alikuwa Waziri wa Nishati na Miundombinu kabla ya kuteuliwa hii leo kuchukua nafasi ya Cohen aliyepelekwa Wizara ya Nishati na Miundombinu.

“Waziri wa sasa wa Nishati, atabadilishana nyadhifa na Cohen kama sehemu ya mzunguko wa mawaziri ambao unategemea idhini ya Bunge,” imeeleza taarifa ya Serikali ya nchi hiyo.

Katz, ambaye hapo awali alishawahi kuhudumu katika wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Nje tangu 2019 hadi 2020, anarudi tena ikiwa ni wakati muhimu kidiplomasia ambapo nchi hiyo inapaswa kudumisha uhusiano wa kimataifa wakati vita vinaendelea.

Kwa upande wa Cohen yeye aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje mwaka jana katika Serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ambayo inachukuliwa kuwa ya mrengo wa kulia zaidi katika historia ya Israel.

Hata hivyo Cohen ataendelea kuhudumu kama mjumbe wa baraza la mawaziri la usalama.

Mabadiliko hayo yanakuja zaidi ya miezi miwili baada ya vita kati ya Israel na Hamas huko Ukanda wa Gaza, iliyotokana na uvamizi wa wanamgambo hao kusini mwa Israel Oktoba, 7 mwaka huu.

Takwimu za Israel zinasema Hamas wameua takriban watu 1,140, wengi wao wakiwa raia huku upande wa Gaza wakifa watu zaidi ya 21,000 hadi sasa.