Israel, Marekani zatofauiana kuhusu Palestina

Muktasari:

  • Israel imepinga msimamo wa muda mrefu wa Marekani juu ya kuundwa kwa taifa la Palestina, kama sehemu ya makubaliano ya kumalizika kwa vita vya Israel, dhidi ya wanamgambo wa Hamas.

Dar es Salaam. Israel imepinga msimamowa muda mrefu wa Marekani juu ya kuundwa kwa taifa la Palestina, kama sehemu ya makubaliano ya kumalizika kwa vita vya Israel dhidi ya wanamgambo wa Hamas.

Shirika la Utangazaji la Sauti ya Marekani (VOA) limeripoti kuwa maofisa kutoka Serikali ya mrengo wa kulia ya Israel pia wameonyesha upinzani wa kuundwa kwa taifa huru la Palestina linalopakana na Israel.

Hata hivyo, hotuba ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kwa wanahabari jana Alhamisi Januari 18, 2024, imeweka wazi tofauti iliyopo kati ya taifa hilo na Marekani, ambaye ni mshirika wake mkuu kwenye vita hivyo.

Hata hivyo, Msemaji wa Baraza la Kitaifa la Usalama wa Marekani, John Kirby amepuuzia matamshi hayo akisema “hili si tangazo jipya kutoka kwa Waziri Mkuu Netanyahu. Hata hivyo tunaliangia kwa mtazamo tofauti.”


Rais wa Marekani, Joe Biden

Chanzo cha uhasama

Tovuti ya Shirika la Habari la Uingereza (BBC) imeripoti kuwa mgogoro kati ya Israel na Palestina umekuwepo kwa takriban miaka 100 sasa na kwamba suala la umiliki wa ardhi ndio limetajwa kuwa nyeti.

Inaelezwa kuwa kuwa Uingereza ilichukua na kudhibiti eneo linalojulikana kama Palestine baada ya mtawala wa eneo hilo la Mashariki ya Kati, Mfalme wa Ottoman kushindwa katika Vita vya Kwanza vya Duniani.

Ardhi hiyo ilikuwa ikimilikiwa na Wayahudi walio wachache na Waarabu walio wengi.

Uhasama baina ya makundi hayo mawili ulianza wakati jamii ya kimataifa ilipoipatia Uingereza jukumu la kuwapatia makazi Wayahudi katika eneo la Wapalestina.

Kwa upande wa Wayahudi, eneo hilo lilikuwa la mababu zao, lakini Waarabu Wapalestina pia nao walidai kumiliki ardhi hiyo na hivyo wakapinga mpango huo.

BBC imeendelea kuripoti kuwa ghasia kati ya Wayahudi na Waarabu na dhidi ya utawala wa Uingereza ziliongezeka.

Mwaka 1947, Umoja wa Mataifa ulipiga kura kwa Palestina kugawanywa kati ya mataifa ya Wayahudi na Wapalestina huku Mji wa Jerusalem ukiwa wa kimataifa.

Mpango huo, ulikubaliwa na Wayahudi huku Waarabu wakiupinga na hivyo haukutekelezwa.


Uanzishaji wa taifa la Israeli

Baada ya kushindwa kutatua mzozo huo, mwaka 1948 watawala wa Uingereza waliondoka na viongozi wa Kiyahudi wakatangaza uanzishwaji wa taifa la Israel, jambo lililopingwa na Wapalestina wengi na hivyo kuanza kwa vita.

Wanajeshi kutoka mataifa jirani ya Kiarabu walivamia, mamia ya maelfu ya raia wa Kipalestina waliyakimbia au kulazimishwa kutoka katika makazi yao.

Mwaka uliofuata baada ya vita kumalizika, Israel ilikuwa ikidhibiti eneo kubwa, huku Jordan ikiteka ardhi iliyojulikana baadaye kama Ukingo wa Magharibi, huku Misri ikilinyakua eneo la Gaza.

Jerusalem iligawanywa kati ya wanajeshi wa Israel waliopo magharibi na wale wa Jordan waliopo mashariki. Na kwa kuwa hakukuwepo kwa mkataba wa amani, kila upande ulilaumu mwingine huku kukiwa na vita zaidi kwa miongo kadhaa.

Katika vita vyingine, inaelezwa kuwa Israel ililiteka eneo la Mashariki mwa Jerusalem na lile la Ukingo wa Magharibi pamoja na eneo kubwa la Milima ya Golan iliyopo Syria, Gaza na rasi ya Sinai iliyopo Misri.

Wakimbizi wengi wa Palestina wanaishi katika eneo la Gaza na Ukingo wa Magharibi pamoja na mataifa jirani ya Jordan, Syria na Lebanon.

Wakimbizi hao na wajukuu wao hawakuruhusiwa na Israel kurudi katika makazi yao, kwani Israel iliamini kuwa hatua hiyo itatishia uwepo wake kama taifa la Wayahudi.

Israel bado inaendelea kulidhibiti eneo la Ukingo wa Magharibi, na ijapokuwa iliondoka katika ukanda wa Gaza, bado Umoja wa Mataifa unalitambua eneo hilo kama eneo lililotekwa.

Israel inadai kumiliki Jerusalem kama Mji Mkuu wa Israel huku Palestina ikidai kuwa Jerusalem ya Mashariki ndio itakayokuwa mji wake mkuu wa taifa lijalo la Kipalestina.

Ni Marekani pekee ndiyo inayotambua kwamba Jerusalem ni eneo la Israel na katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, Israel imekuwa ikijenga makazi katika maeneo hayo ambapo takriban raia 600,000 wa Kiyahudi wanaishi.

Palestina inasema makazi hayo ni haramu na kinyume na sheria ya kimataifa na kikwazo cha kuleta amani, lakini Israel imekuwa inalipinga suala hilo.

Wasiwasi juu

BBC inaendelea kuhabarisha kuwa hali ya wasiwasi ipo juu kati ya raia Israel na Wapalestina wanaoishi Mashariki mwa Jerusalem, katika eneo la Gaza na lile la Ukingo wa Magharibi.

Gaza inatawaliwa na kundi la wapiganaji wa Kipalestina kwa jina la Hamas, ambalo lilipigana na Israel mara nyingi.

Israel na Misri wanadhibiti eneo la mpakani la Gaza ili kuzuia silaha kusafirishwa kwenda kwa wapiganaji wa Hamas.

Raia wa Palestina wanaoishi Gaza pamoja na Ukingo wa Magharibi wanasema wanateseka kutokana na vitendo vya Israel na vikwazo.

Israel nayo inasema kuwa inatekeleza vitendo hivyo ili kujilinda dhidi ya ghasia za Palestina. Kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, kumekuwa na ghasia katika mpaka wa Gaza na Israel.

Raia wa Palestina wamekuwa wakifanya maandamano, wakiwataka wakimbizi kurudi kwenye makazi yao katika eneo ambalo sasa ni la Israel.

Israel inasema waandamanaji hao wanatumika kama ngao ili kuwashambulia.

Makumi ya raia wa Kipalestina wameuawa na wanajeshi wa Israel ambao wanasema wanachukua hatua hiyo kujilinda.

Hakuna muafaka

Kuna masuala kadhaa ambayo Israel na Palestina hawawezi kukubaliana, haya ni kama vile nini hatima ya wakimbizi wa Palestina, iwapo makazi ya Wayahudi ya Ukingo wa Magharibi yanafaa kuondolewa au yaachwe.

Lakini pia kuna suala la iwapo wawili hao wanafaa kutumia kwa pamoja Mji wa Jerusalem na pengine kubwa zaidi ni iwapo taifa la Palestina linaweza kuundwa kama lilivyo lile la Israel.

Mazungumzo ya amani yamekuwa yakifanyika kwa zaidi ya miaka 25 sasa, lakini kufikia sasa hakuna suluhu ya mzozo huo.

Nini hatima ya mzozo

Kwa mujibu wa BBC, hatima juu ya mzozo huo haiwezi kupatikana hivi karibuni, hata hivyo, mpango mpya wa amani unaandaliwa na Marekani ambayo imeutaja kuwa mpango mzuri wa karne hii.

Hakuna anayejua kilicho ndani yake, lakini Marekani inasema kuwa huenda ikautangaza mpango huo mwezi Mei au Juni 2019.

Hata hivyo, Wapalestina wanasema Marekani inaipendelea Israel na hivyo hawatakubali mpango wowote utakaoandaliwa na Marekani, lakini Israel inasema itasubiri kuona ni mpango gani ilia ma ikubali au la.

Iwapo mpango huo utafanikiwa, utamaliza mojawapo ya mizozo mikubwa zaidi duniani, lakini ukishindwa vita vitaendelea.