Dk Tulia aanza kusaka mwarobaini mgogoro wa Israel, Palestina

Muktasari:

  • Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dk Tulia Ackson ameanza kutekeleza majukumu yake kwa kuagiza Kamati ya Masuala ya Mashariki ya Kati ya umoja huo kuanza kutafuta mwarobaini wa kurejesha amani Israel na Palestina.

Dar es Salaam. Siku chache baada ya kuchaguliwa, Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dk Tulia Ackson ameagiza Kamati ya Masuala ya Mashariki ya Kati ya umoja huo kuanza kutafuta suluhu ya mgogoro kati ya Israel na Palestina.

Dk Tulia ambaye pia ni Spika wa Bunge la Tanzania, ametoa agizo hilo leo Novemba 30, 2023 jijini Tel Aviv, Israel baada ya kumaliza ziara ya kikazi ya siku mbili iliyompa fursa ya kufanya mazungumzo na viongozi wa Israel na mamlaka ya Palestina.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma, Dk Tulia ameagiza kamati hiyo kuhakikisha amani na usalama vinapatikana kutokana na mgogoro unaoendelea kati ya Israel na Palestina.    

“Nimekuja kutembelea maeneo ya Palestina na Israel ambao wote hawa mabunge yao ni wanachama wa IPU.

“Lakini muhimu zaidi kuwafahamisha kuwa tupo pamoja katika kipindi hiki kigumu na kamati hiyo itakuwa hapa siku zijazo kutafuta uhalisia wa mgogoro na kuleta taarifa tutakayoijadili ili tuone huko mbele tunawezaje kuwa na amani na usalama kwa watu wote," amesema Dk Tulia.

Amesema miongoni mwa msingi ya IPU ni kuhakikisha uhai wa kila binadamu unalindwa na IPU itafanya kila linalowezekana ili dunia iwe sehemu salama na ya amani kwa binadamu wote bila kujali rangi, itikadi, imani na maeneo wanayotoka.

Aidha, amesisitiza mpango mkakati wa umoja huo mwaka 2024 ni kujadili kwa kina suala la amani na usalama kama ajenda muhimu kwenye mikutano yake mikuu ya Machi na hadi Oktoba mwakani.

Dk Tulia ametembelea Kijiji cha Kfar Aza Kibbutz kati ya vijiji vilivyoshambuliwa na wanamgambo wa Hamas Oktoba 7, 2023 na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Israel (Knesset) Amir Ohana, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Vijiji, Avi Dicter na wabunge wa Knesset kwenye IPU.