Kagame kugombea tena urais Rwanda

Rais wa Rwanda Paul Kagame akisisitiza jambo.Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Kagame amekuwa Rais wa Taifa hilo la Afrika Mashariki tangu mwaka 2000. Kura ya maoni iliyozua utata mwaka 2015 iliondoa ukomo wa mihula miwili ya kikatiba kwa marais.

Kigali. Rais wa Rwanda, Paul Kagame amesema atawania muhula wa nne katika uchaguzi wa Rais utakaofanyika mwaka ujao.

“Ndiyo, hakika mimi ni mgombea,” Kagame aliliambia jarida la lugha ya Kifaransa la Jeune Afrique Jumanne iliyopita kama ilivyonukuliwa pia na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Alipoulizwa kuhusu nchi za Magharibi zitachukulia vipi uamuzi wake wa kugombea tena, Rais Kagame alisema, “Samahani kwa nchi za Magharibi, lakini kile ambacho nchi za Magharibi hufikiri si tatizo langu”.

“Nimefurahishwa na imani ambayo Wanyarwanda wanayo kwangu. Nitawatumikia daima, kadri niwezavyo.”

Rais Kagame alitania Aprili 2023 kwamba anatazamia kustaafu na kukabidhi madaraka baada ya miaka 23 madarakani.

Chama tawala nchini humo cha Rwandan Patriotic Front (RPF-Inkotanyi), kilimuacha Kagame kuendelea kuhudumu kama mwenyekiti wake Aprili. Ameongoza chama hicho tangu mwaka 1998.

Kagame amekuwa Rais wa Taifa hilo la Afrika Mashariki tangu mwaka 2000. Kura ya maoni iliyozua utata mwaka 2015 iliondoa ukomo wa mihula miwili ya kikatiba kwa marais.

Alishinda uchaguzi uliopita wa mwaka 2017 kwa asilimia 98.8 ya kura.

Rwanda chini ya Rais Kagame imekuwa na utulivu wa kisiasa lakini wakosoaji na makundi ya haki za binadamu yanaituhumu Serikali yake kwa kuweka mipaka ya uhuru wa kisiasa na kukandamiza upinzani.