Kigogo wa Marekani kukutana na Israel

Muktasari:

  • Ziara yake itajikita kuzungumzia vita vinavyoendelea kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas

Israel. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken leo Januari 9, 2024 anatarajia kukutana na viongozi wa Israel ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuzuia vita huko Gaza.

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya ndege za kivita kushambulia nchini Syria na Lebanon na kuwaua wanachama mashuhuri wa Hamas na mshirika wake Hezbollah.

Ziara hiyo inajiri huku jeshi la Israel likisema kampeni yake dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza inaelekea katika awamu mpya inayohusisha operesheni zinazolengwa zaidi katikati mwa eneo hilo na kusini.

Ving'ora vya kuonya kuhusu roketi zinazoingia kati na kusini mwa Israel vilisikika siku ya Jumatatu na maeneo yaliyo karibu na mpaka na Lebanon ambapo mashambulizi ya Israel na kurushiana risasi na wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran yalikuwa yakiendelea na kuzusha hofu kwamba vita hivyo vinaweza kuenea kaskazini.

Mapema kundi la Hezbollah lilitangaza kuuawa kiongozi wa kijeshi, Wissam Hassan Tawil kwa mara ya kwanza tangu Oktoba mwaka jana.

Viongozi wa ulinzi nchini Lebanon, walieleza Tawil alikuwa na jukumu la kuongoza shughuli za Hezbollah katika maeneo ya kusini na aliuawa kwa mashambulizi ya ndege za kijeshi za Israel.

Taarifa ya jeshi la Israel ilisema walifanya mashambulizi katika maeneo ya Hezbollah nchini Lebanon jana lakini haikuelezea kuhusu kifo cha Tawil.

Tawil ni kiongozi wa pili wa juu kuuawa mwezi huu, baada ya kifo cha Saleh al-Aruri kilichotokea nchini Lebanon kutokana na mashambulizi ya ndege za kivita katika mji wa Beirut ambako ni ngome ya Hezbollah.

Taarifa ya jeshi la Israel pia imesema imemuua kiongozi muhimu wa Hamas nchini Syria, Hassan Akasha ambaye alikuwa akiratibu urushaji wa roketi katika maeneo ya Israel.

Mashambuli ya Israel yanaendelea eneo la Gaza ikiwa ni sehemu ya kulipa kisasi kutokana na kile kilichotokea Oktoba 7, 2023 baada ya kundi la Hamas kushambulia Israel na kuua watu 1,140 nchini wengi wao wakiwa raia.

Hamas pia waliwateka watu 250, baadhi yao iliwaachia huru huku 132 wakiendelea kuwashikilia hadi sasa, 25 wakiaminika kuuawa.

Kutokana na shambulio hilo, Israel walijibu mapigo kwa kushambulia maeneo mbalimbali eneo la Gaza na kuua watu 23,084 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.

Mwisho.