Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kitendawili kipya mazungumzo ya Iran, Marekani Doha

Muktasari:

  • Mazungumzo ya Doha yaliyotangazwa kurejesha mawasiliano ya Iran na Marekani yamegubikwa na kauli kinzani, Trump akithibitisha mkutano huku Tehran ikikanusha kuwepo kwa mazungumzo hayo.

Dar es Salaam. Kitendawili kipya kimeibuka kuhusu mustakabali wa mazungumzo kati ya Iran na Marekani baada ya kauli zinazokinzana kuhusu mkutano uliodaiwa kupangwa kufanyika Doha, Qatar, hali inayozidisha sintofahamu ya kidiplomasia katika Ghuba ya Uajemi.

Kinachoendelea ni mvutano wa taarifa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kudai kupitia mtandao wa Truth Social kwamba Iran imeomba mazungumzo na kwamba mkutano ungefanyika Doha leo Jumanne Juni 30, 2026, kauli iliyosambaa pia katika baadhi ya vyombo vya habari vya kimataifa. Hata hivyo, Iran imekanusha moja kwa moja taarifa hizo.

Kwa mujibu wa Reuters, Marekani ilisema mazungumzo yalikuwa yamepangwa kupitia wapatanishi lakini Iran imesisitiza hakuna mazungumzo ya moja kwa moja yaliyokubaliwa na pande zote mbili.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Kazem Gharibabadi amenukuliwa na vyombo vya habari nchini humo akisema:“Hakuna mazungumzo ya kitaalamu yaliyopangwa wiki hii na hakuna makubaliano ya mkutano na Marekani,” akisisitiza mawasiliano ni ya kupitia wapatanishi pekee.

Hatua hii inaibua sintofahamu na hofu ya mapigano mapya ikiwa Rais Trump alisisitiza umuhimu wa mazungumzo hayo akiweka wazi kuwa yatakuwa Doha na Marekani ikikosa uvumilivu kwa kupuuzwa mazungumzo Iran itashambuliwa vibaya, kabla ya Tehran kukanusha kwa kusema hakuna ratiba rasmi ya mkutano wowote na Marekani.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia imeeleza kuwa ujumbe wake uliokwenda Qatar unahusiana na suala la mali za Iran zilizogandishwa nje ya nchi, si mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani.

Awali, kulikuwa na mpango wa wapatanishi kuandaa mkutano Doha kama sehemu ya kurejesha mazungumzo ya amani baada ya mapigano na mvutano mpya katika eneo la Hormuz.

Mpango huo ulihusisha pia makubaliano ya muda yaliyosainiwa Juni 17, 2026 ambayo yalilenga kusitisha na kufungua njia ya mazungumzo ya kudumu, yaliyokuwa na vipengele muhimu ikiwemo, kusitisha mashambulizi  kati ya pande mbili, kuhakikisha usalama wa usafiri katika Mlango wa Hormuz, kuanzisha mazungumzo ya nyuklia kwa hatua, na kuanza kufunguliwa kwa baadhi ya mali za Iran zilizozuiwa.

Hata hivyo, makubaliano hayo yalianza kuyumba baada ya mashambulizi mapya ya baharini na tofauti kuhusu nani anadhibiti usalama wa Hormuz. Iran ilisisitiza kuwa usimamizi wa mlango huo ni wake pekee, kauli iliyopingwa na mataifa ya Magharibi.

Katika hatua nyingine, Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alisisitiza haja ya ushirikiano wa kimataifa katika usalama wa bahari, lakini Iran ilijibu kwa kusema hatua hiyo ni uingiliaji wa mamlaka yake ya ndani.

Umoja wa Mataifa, ambao awali ulijaribu kuratibu mazungumzo hayo na kusimamia shughuli za uokoaji Hormuz, ilisitisha ushiriki wake kutokana na kuibuka kwa mashambulizi mapya ambapo Iran ilihusishwa na shambulizi la meli ya mizigo  Hormuz wiki iliyopita.

Kusuasua kwa mwafaka katika ukanda huo, soko la mafuta limeendelea kuathirika na kuzua hofu ya bei duniani katika hatua tofautitofauti zinazoendelea.

Kwa mujibu wa taarifa za masoko zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya kimataifa, bei ya mafuta ilipanda wakati wa mashambulizi kutoka takribani Sh191,000 hadi takriban Sh312,000 kwa pipa na baadaye kushuka hadi Sh250,000 baada ya dalili za kumalizika mzozo huo katika mazungumzo ya awali.

Bei hizo zinadaiwa kwa sasa kupanda tena hadi karibu Sh295,000 kwa pipa kutokana na sintofahamu ambayo imeendelea kujitokeza.

Kauli kinzani kuhusu mkutano wa Doha uliotazamiwa kurejesha mazungumzo  na kupunguza mvutano Hormuz, leo zimefifisha matarajio hayo ya matumaini ya kushuka kwa bei ya nishati hiyo.Hali hii  ya sasa inaonyesha pengo  la kuaminiana kati ya Washington na Tehran.