Lori la gesi lalipuka, watatu wafariki dunia, zaidi ya 200 wajeruhiwa

Muktasari:

  • Lori la gesi limelipuka na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Nairobi, Kenya. Watu watatu wamefariki dunia na wengine zaidi ya 280 kujeruhiwa katika moto mkubwa uliotokana na lori la gesi kulipuka katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi usiku wa kuamkia leo Ijumaa Februari 2, 2024.

Mlipuko huo uliwasha moto mkubwa ulioenea sana, Isaac Maigua Mwaura, msemaji wa Serikiali amesema kwenye mtandao  wa X.

"Kwa sababu hiyo, moto huo umeharibu zaidi magari na mali kadhaa za biashara ndogo na za kati," amesema Mwaura na kuongeza kuwa "nyumba za makazi katika eneo hilo zimeteketea kwa moto na idadi kubwa ya wakazi bado wako ndani kwa kuwa ulikuwa usiku mnene."

Watu watatu wamefariki dunia kutokana na majeraha  na wengine 280 walipelekwa kwenye hospitali mbalimbali katika mji wa Nairobi, msemaji wa serikali amesema.

Hapo awali, Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya lilikuwa limeripoti karibu watu 300 wamejeruhiwa katika  moto huo.

Mnamo saa 7:00, maofisa wa Zimamoto walikuwa bado wanafanya jitihada za kuudhibiti moto huo, kwa mujibu wa mwandishi wa Shirika la Habari la Ufaransa, AFP.

Moshi mkubwa mweusi uliosimama mithiri ya nguzo ulionekana kufuka kutoka eneo hilo ambalo askari polisi walikuwa wakililinda.Mlipuko mkubwa
Moto huo ulizuka usiku wa kuamkia leo katika eneo la Embakasi, kusini mashariki mwa Nairobi.

Picha zilizorushwa na vyombo vya habari vya ndani zilionyesha moto mkubwa karibu na nyumba kadhaa za eneo hilo.

Kulingana na mwandishi wa habari wa AFP, nyumba nyingi na magari viliteketea.

"Tulikuwa ndani ya nyumba na tukasikia mlipuko mkubwa," James Ngoge, anayeishi kando ya barabara karibu na mahali moto ulipotokea, aliieleza AFP.

"Jengo lote lilitikisika kwa tetemeko kubwa, nilihisi litaanguka. Mwanzoni hata hatukujua kinachoendelea, ilikuwa ni kama tetemeko la ardhi.

"Nina biashara barabarani na imeharibiwa kabisa," amesema.

Wakazi wengi wa eneo hilo walilala nje usiku kucha kufuatia ajali hiyo.

Polisi wamezingira eneo lililoathiriwa, lakini baadhi ya watu walionekana wakikusanya mali zao na kuangalia kiasi cha uharibifu.