Mahakama Afrika Kusini yamsafishia njia Zuma kugombea urais

Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Jacob Zuma akiondoka katika Mahakama ya uchaguzi mjini Johannesburg, Aprili 8, 2024. Picha ya AFP

Muktasari:

  • Uamuzi huo unampa mwanya Jacob Zuma kugombea muhula mwingine wa uongozi katika Taifa hilo kupitia chama cha Umkhonto weSizwe, au MK.

Johannesburg. Mahakama ya Uchaguzi nchini Afrika Kusini imeamua aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma kugombea muhula mwingine katika uchaguzi wa mwezi ujao na kubatilisha uamuzi uliomwekea kikwazo kiongozi huyo kugombea.

 Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Shirika la Habari la Marekani (AP) kwa uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo jana Jumanne, April 9,2024  hatua hiyo inampa mwanya Zuma kugombea muhula mwingine wa uongozi katika Taifa hilo.

Rais Zuma atagombea nafasi hiyo ya juu nchini humo kupitia chama cha Umkhonto weSizwe, au MK, chama kipya ambacho kiongozi huyo alijiunga nacho baada ya kukikacha chama chake cha ANC.

Wananchi wa Afrika kusini watawachagua wajumbe 400 wa Baraza Kuu la nchi Mei 29, 2024 mwezi mmoja baadaye, wabunge katika bunge jipya watachagua rais wa nchi hiyo.

Tume huru ya uchaguzi nchini humo ilimtengua Zuma kutogombea nafasi hiyo kwa mara nyingine kutokana na rekodi zake za uhalifu, baada ya kupokea mapingamizi juu ya uhalali wa kiongozi huyo kugombea.

Katiba ya Afrika Kusini haimruhusu mtu anayetuhumiwa na uhalifu na kuhukumiwa gerezani zaidi ya miezi 12 bila kupewa njia mbadala ya kulipa faini kuwania uongozi.

Zuma alikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miezi 15 jela mwaka 2021 kwa kukaidi agizo la Mahakama la kufika mbele ya tume ya mahakama iliyohusika kuchunguza tuhuma za ufisadi katika Serikali na kampuni zinazomilikiwa na Serikali wakati wa utawala wake kuanzia 2009 hadi 2018.

Hata hivyo, katika amri ya Mahakama iliyotolewa jana Jumanne, Mahakama ilitangaza kuwa rufaa ya Zuma na chama chake ilifanikiwa na kwamba pingamizi dhidi ya kugombea kwake limetupiliwa mbali.

Kutokana na uamuzi huo, chama cha uMkhonto weSizwe cha kiongozi huyo, kilikaribisha uamuzi wa Mahakama, kikisema uamuzi wa tume ya uchaguzi wa kumzuia Zuma kugombea ulikuwa mbaya.

Kwa mujibu wa msemaji wake, Nhlamulo Ndhlela, kiongozi huyo atajitokeza kwenye kinyang’anyiro kama mgombea wa urais wa chama hicho.

“Tumefurahishwa na uamuzi wa Mahakama kwa sababu tumekuwa tukisema Rais Zuma na haki za chama cha MK," amesema Ndhlela.

Ameongeza:"Hii inamaanisha nini kimsingi ni kwamba atakuwa mgombea wetu wa urais na atakuwa bungeni baada ya uchaguzi."

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Dirk Kotze, kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini, amesema Zuma huenda akatumia ushindi wake wa kimahakama kuendeleza hoja yake kwamba marufuku ya awali ya kugombea uchaguzi ni sehemu ya kampeni za kisiasa dhidi yake.

Uchaguzi mkuu wa Afrika Kusini unatarajiwa kuwa wenye ushindani mkali tangu ujio wa demokrasia mwaka 1994 na kuwepo kwa Zuma katika kampeni inaweza kuwa kichocheo cha ushindani huo.

Kikitegemea umaarufu wa Zuma, chama cha MK kinatarajiwa kugawana kura na chama tawala cha African National Congress, makao ya kisiasa ya rais huyo wa zamani.

Katika uchaguzi huo, Rais wa sasa wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa aliyeingia madarakani mwaka 2019 baada ya Zuma kujiuzulu, atatetea kiti chake kwa muhula wa pili.

Imeandikwa na Baraka Loshilaa kwa msaada wa mashirika ya kimataifa