Mahakama yabariki ushindi wa Tinubu Nigeria

Lagos. Mahakama nchini Nigeria, imeidhinisha matokeo ya kura za urais, yaliyomwingiza madarakani Rais Bola Tinubu, kwa kutupilia mbali rufaa ya kesi hiyo ikisema "haikuwa na sifa."
Rais huyo alichaguliwa katika uchaguzi uliokuwa na ushindani Februari mwaka huu, ambapo wagombea walioshindwa walikimbilia mahakamani kupinga matokeo hayo wakisema ulikuwa na dosari.
Atiku Abubakar mgombea wa People's Democratic Party, na Peter Obi wa Labour Party, walikuwa wamedai ukiukaji wa sheria za uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kutokutumika mashine za kielektroniki kujaza matokeo ya vituo vya kupigia kura.
Hata hivyo, majaji wametupilia mbali madai hayo kuwa "hayafai."
"Ni dhahiri kwamba walalamikaji wameshindwa kuthibitisha," amesema Haruna Tsammani, mkuu wa jopo hilo na kuongeza; "Hawajaweza kutoa ushahidi wowote unaokubalika, unaoaminika na unaokubalika."
DW imeripoti kuwa uamuzi huo unatarajiwa kupelekwa katika Mahakama ya Juu, ambapo Abubakar na Obi wanaweza kukata rufaa ndani ya siku 60.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa Mahakama ya juu haijawahi kutoa uamuzi wa kutengua matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Nigeria tangu nchi hiyo irejee kwenye demokrasia kutoka kwa utawala wa kijeshi mwaka 1999.
Katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali wa Februari 25, aliyekuwa Gavana wa Lagos, Tinubu alipata asilimia 37 ya kura, akiwapita Atiku Abubakar wa PDP na Peter Obi wa Labour.
Vyama vya PDP na Labour katika kesi zao tofauti zinataka matokeo ya kura kutupiliwa mbali na wagombeaji wao watangazwe washindi au mahakama iitishe uchaguzi wa marudio.
Na ili kuwe na uwazi, vyama hivyo viliitaka Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (INEC), kutumia teknolojia ya kibayometriki na IReV, wakati wa kuhesabu matokeo katika muda halisi.
Hata hivyo, japo INEC inakiri kulikuwa na "makosa" lakini ikakanusha madai kwamba uchaguzi huo ulihujumiwa.