Makamu wa Rais Malawi, wengine tisa wafariki dunia ajali ya ndege

Muktasari:

  • Ndege hiyo iliondoka Lilongwe saa 3:17 asubuhi jana Juni 10, 2024 na ilipangwa kutua Uwanja wa Ndege wa Mzuzu saa nne asubuhi.

Blantyre. Rais wa Malawi, Dk Lazarus Chakwera ametangaza kupatikana ndege ya Jeshi la Malawi iliyokuwa imembeba makamu wa Rais wa nchi hiyo, Saulos Klaus Chilima (51) ikiwa imepata ajali katika msitu wa Chikangawa.

"Ndege imepatikana, na nimehuzunishwa sana na ninasikitika kuwajulisha wote. Imekuwa mkasa mbaya," amesema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari leo.

Ndege hiyo iliondoka Lilongwe saa 3:17 asubuhi jana Juni 10, 2024 na ilipangwa kutua Uwanja wa Ndege wa Mzuzu saa nne asubuhi, lakini haikuweza kutua kutokana na hali ya hewa na kuamriwa kurejea katika mji mkuu.

Hata hivyo, mamlaka ya usafiri wa anga nchini humo ilishindwa kuwasiliana na ndege hiyo tangu ilipotoka kwenye rada.

Mabaki ya ndege ya jeshi iliyokuwa imembeba Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Klaus Chilima ikiwa imeanguka katika msitu wa Chikangawa.

Kwa mujibu wa Zamba, utafutaji wa ndege hiyo uliozinduliwa jana baada ya taarifa ya kupotea umefanywa na Jeshi la Ulinzi la Malawi, Jeshi la Polisi na Idara ya Usafiri wa Anga.

“Rais Dk Lazarus Chakwera ametaarifiwa kuhusu tukio hilo na ametoa salamu zake za rambirambi kwa familia ya Makamu wa Rais na wengine waliopoteza wapendwa wao." inasema taarifa hiyo.

Awali, Shirika la Habari la Reuters lilimnukuu Ofisa Mkuu wa Jeshi Paul Phiri akisema utafutaji na uokoaji ulikuwa ukiendelea ndani ya msitu huo wa Chikangawa huku hali ya hewa ya ukungu ikizunguka.

Katika taarifa nyingine, Rais wa nchi hiyo Lazarus Chakwera amesema tayari amewasiliana na Serikali za mataifa ya Marekani, Uingereza, Norway na Israel kutoa msaada wa kutafuta ndege hiyo.

Taarifa ya Serikali ya nchi hiyo ikinukuliwa na Shirika la Habari la AFP, nchi hizo zote za kimataifa zimetoa msaada kwa nyadhifa tofauti ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia maalumu itakayoongeza uwezo wa kuipata ndege hiyo mapema.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku 22 tangu helikopta iliyokuwa imembeba Rais wa Iran, Ebrahim Raisi kuanguka baada ya kupata shida katika kutua kabla ya kuripotiwa kufariki dunia Aprili 20, 2024.

Kwa mujibu wa Televisheni ya Taifa ya Iran, helikopta hiyo ilianguka karibu na Mji wa Jolfa, uliopo mpakani na Taifa la Azerbaijan.

Alifariki dunia wakati akiwa ametoka kuzindua bwawa na Rais wa taifa hilo, Ilham Aliyev ikiwa ni la tatu kujengwa na mataifa hayo mawili kwenye Mto Aras.

Aprili 18, 2024 helikopta iliyokuwa imembeba Mkuu wa Majeshi na Vikosi vya Ulinzi ya Kenya, Meja Jenerali Francis Ogolla na maofisa wengine tisa ilianguka na kulipuka eneo la Cheptulel lililopo Kaunti ya West Pokot.

Katika ajali hiyo watu watano walifariki dunia, akiwamo Meja Jenerali Ogolla.


Imeandaliwa kwa msaada wa Mashirika ya habari.