Ndege ya Jeshi iliyombeba Makamu wa Rais wa Malawi yatoweka

Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Klaus Chilima.

Muktasari:

  • Mamlaka za nchini Malawi zimethibitisha kupotea angani kwa ndege iliyokuwa imembeba Makamu wa Rais na watu wengine tisa.

Dar es Salaam. Ndege ya Jeshi la Ulinzi la Malawi iliyokuwa imembeba Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Klaus Chilima na watu wengine tisa imetoweka na kutokomea kusikojulikana.

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Juni 10, 2024 kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Rais wa Malawi.

"Juhudi zote za mamlaka ya usafiri wa anga kuwasiliana na ndege tangu iliporuka kwenye rada zimeshindwa hadi sasa," imesema taarifa ya Ofisi ya Rais na Baraza la Mawaziri.

Chilima (51), alikuwa ndani ya ndege ya Jeshi la Ulinzi la Malawi iliyoondoka katika mji mkuu Lilongwe saa 09:17 asubuhi na hadi sasa haijapatikana, huku wakiongeza juhudi za utafutaji na uokoaji.

Ndege hiyo ilikuwa imepangwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzuzu, saa 10:02 asubuhi, kwa mujibu wa taarifa hiyo.