Mapinduzi yazimwa kama yalivyoanza-7

Mwanajeshi Private Hezekiah Ochuka

Muktasari:

  • Katika toleo lililopita tuliangazia jinsi mtangazaji maarufu wa redio, Leonard Mambo Mbotela alivyotekwa na wanajeshi nyumbani kwake, akapelekwa kituo cha Redio ya Sauti ya Kenya (VoK) na kulazimishwa kutangaza kuwa, Serikali ya Rais Daniel Arap Moi imepinduliwa na jeshi.

Katika toleo lililopita tuliangazia jinsi mtangazaji maarufu wa redio, Leonard Mambo Mbotela alivyotekwa na wanajeshi nyumbani kwake, akapelekwa kituo cha Redio ya Sauti ya Kenya (VoK) na kulazimishwa kutangaza kuwa, Serikali ya Rais Daniel Arap Moi imepinduliwa na jeshi.


Wakati Private Hezekiah Ochuka na Sajenti Pancras Oteyo Okumu wakidhibiti kituo cha VoK, mitaani risasi zilikuwa zinarindima huku raia wakiwa hawana silaha nzito za kupambana na wanajeshi wanaoitii Serikali ya Moi.

Aliyepewa jukumu la kuvamia VoK ni Sajenti Okumu ambaye alilitekeleza saa nane usiku.

Wakati kukiwa na milio ya risasi, Sajenti Okumu aliondoka kuelekea Kambi ya Jeshi la Anga la Kenya (KAF) ya Eastleigh, alikoamini angekuwa salama. Saa tisa alfajiri alirudi studio za VoK kuungana na Ochuka.

“Tunapaswa kupata ndege kutoka Nanyuki kuja Nairobi na ikiwezekana kulipua studio za VoK, Ikulu na makao makuu ya polisi,” Ochuka alimwambia Okumu ambaye bado alikuwa amepigwa na butwaa.

Walipiga simu Kambi ya Jeshi ya Nanyuki na baada ya muda ndege zilifika Nairobi. Hatua hiyo ilitokana na simu za hasira alizopiga Ochuka, aliyetaka maeneo fulani ya kimkakati kupigwa mabomu.

Maeneo hayo ni VoK, Ikulu, makao makuu ya polisi na Kambi ya Langata.

Siku mbili kabla ya mapinduzi, Mkuu wa Usalama wa Taifa, James Kanyotu alimwomba Rais Moi ruhusa ya kuwakamata wanajeshi kama Sajenti Joseph, Koplo Charles Oriwa, Walter Ojode, Bramwel Injene Njereman, Okumu na Ochuka, lakini Moi hakutilia sana maanani.

Usiku wa tukio hilo, Kapteni Jorim Nyamor alikuwa nyumbani kwake Nairobi wakati mfanyakazi mwenzake, Koplo Rono alipovamia akiwa na bunduki na kutishia kumuua kama asingetii amri zake.

Koplo Rono alimpeleka kwenye kikosi katika kituo chao cha kazi huko Nanyuki ambako Kapteni Nyamor aligundua kuwa wenzake wengi walikuwa wamekamatwa na kuwekwa humo.


Serikali kupinduliwa

Ilikuwa ni saa chache tu baada ya tangazo kutolewa kupitia VoK kwamba, jeshi limepindua Serikali. Tangazo hilo lililotolewa na mtangazaji Mbotela kwa amri ya Ochuka liliungwa mkono mara moja na kiongozi wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Titus Adungosi.

Katika Chuo Kikuu cha Kenyatta kilicho nje kidogo ya jiji, habari za mapinduzi zilipokewa kwa shangwe kubwa, lakini hawakujaribu kujiingiza kwenye ghasia za uporaji.

Wanafunzi wa Shule ya Udaktari ya Kenyatta waliojaribu kufika katikati ya Jiji la Nairobi waligeuka na kurudi nyuma baada ya kukutana na vizuizi vya barabarani vilivyowekwa na polisi na wanajeshi waliomtii Moi.

Katikati ya jiji, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi walijiunga katika uporaji wa maduka mitaani.

Biashara zilizomilikiwa na raia wenye asili ya Asia zililengwa mahususi. Wanajeshi waasi waliteka nyara magari na mabasi madogo ili kubeba mali walizopora.


Njama za kulipua Ikulu

Katika kikosi cha Nanyuki kulikuwa na maofisa 20, wengi wao wakiwa marubani ambao baadaye wangetumwa kupiga mabomu kambi tofauti na Ikulu.

Aliyekuwa akiongoza njama za kuilipua Ikulu ya Nairobi na makao makuu ya polisi mjini ni Koplo Bramwel Injeni Njereman aliyewalazimisha marubani watatu (Meja David Mutua, Kapteni John Mugwanja na Kapteni John Baraza) kurusha ndege mbili aina ya ‘F-5E Tiger’ na ‘Strikemaster’ ambazo zingetumika katika operesheni hiyo.

Ndege ya ‘F-5E Tiger’ ya Meja Mutua yenye viti viwili ilipakiwa mabomu huku ndege ya ‘Strikemaster’ ya Kapteni Baraza ikiwa na roketi za kulipuka.

Marubani hao watatu walichukuliwa kwa mtutu wa bunduki kutoka kwenye makazi yao huku Koplo Njereman akiwapa amri ya kwenda kulipua Ikulu ya Nairobi na makao makuu ya polisi.

Koplo Njereman mwenyewe alikaa kiti cha nyuma kwenye ndege nyuma ya Meja Mutua ili kusimamia utekelezaji wa mpango huo.

Licha ya kusimamia njama za kwenda kuilipua Ikulu ya Nairobi kwa kutumia ndege ya jeshi, Koplo Njereman hakuwahi kusafiri kwa ndege, achilia mbali kuongoza njama kubwa kiasi hicho cha kuipindua Serikali na kutumia ndege kuilipua Ikulu.

Marubani walikuwa wakiwasiliana kwa njia ya siri, walikubali kutekeleza amri za waasi kwa ujanja ili kumvuruga Koplo Njereman. Ujanja huo ulifanya kazi, walitupa mabomu katika msitu wa Mlima Kenya wakijifanya wameilipua Ikulu na kurudi Kambi ya Nanyuki.

Kulipokuwa kunapambazuka wanajeshi walivamia ukumbi wa disko karibu na kambi yao kwenye ukingo wa kusini-mashariki mwa Nairobi.

Katika kujaribu kukwepa milio ya risasi, baadhi ya watu waliokuwa wakisherehekea kwenye ukumbi huo usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili walikimbilia kituoni kwenda kuwaita polisi.

Maofisa wa polisi kutoka kituo cha eneo hilo waliitikia mwito na kuzidiwa nguvu na wanajeshi wa KAF waliokuwa na silaha walizozichukua kutoka kwenye ghala.

Wanajeshi waasi waliotoka Embakasi waliteka minara ya kuongozea ndege katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta na Uwanja Mdogo wa Wilson.

Baadaye waliiteka Ofisi Kuu ya Posta na asubuhi wakawa wamesambaa maeneo mengi ya Jiji la Nairobi kuanzia Embakasi kusini hadi Eastleigh mashariki na Barabara ya Ngong upande wa magharibi.

Kwa vile hawakuwa na magari, walitarajia makamanda wao kuiba magari ili wayatumie.

Walivunja vioo na milango ya maduka ya kuuzia magari na kuiba magari hayo. Raia nao waliungana na wanajeshi kupora madukani.

Vikosi vya usalama vilivyoitii Serikali vilikuwa tayari vimeanza kujibu mapigo uporaji ulipoanza. Licha ya kuwapo kwa hali ya kutoridhika miongoni mwa wanajeshi wa KAF, Moi alikuwa amehakikisha kwamba makamanda na maofisa wakuu katika vikosi vingine wameteuliwa kwa uangalifu, kulipwa ipasavyo na kutendewa haki.

Ndani ya saa moja baada ya mapinduzi kuanza, waasi walikuwa wakishambuliwa kwa silaha nzito katika vituo vyote viwili vya KAF mjini Nairobi.

Nje ya jiji, wanajeshi walioitii Serikali katika kambi ya jeshi huko Gilgil, walipelekwa haraka hadi Nanyuki, kaskazini-magharibi mwa Mlima Kenya ili kuzuia marubani wa ndege za KAF walioko huko kujiunga na mapinduzi.

Baada ya kushambuliwa na vikosi vya usalama vilivyoitii Serikali, wanajeshi waasi waliokuwa katika studio za redio za VoK walishindwa ilipofika saa nne asubuhi.

Baadhi ya wanajeshi waasi waliuawa katika kituo hicho cha redio. Saa moja baadaye, ulitangazwa ujumbe redioni kuwa mapinduzi yalikuwa yameshindwa na Moi bado yuko madarakani.

Hadi kufikia alasiri ikabainika kuwa mapinduzi yameshindwa na uporaji ulikoma. Rais Moi alisikika redioni akiwahakikishia Wakenya kuwa, maradaka yake yamerejeshwa.

Je, ni watu wangapi waliuawa katika jaribio hilo? Nini kiliwakuta waliopanga njama hizo?

Tukutane kesho.