Mipango ya kupindua serikali ya Moi yaanza-5

Rais Daniel arap Moi

Muktasari:

  • Katika matoleo yaliyopita tuliangalia namna baadhi ya wanasiasa wa Kenya, wanafunzi wa elimu ya juu na wahadhiri wa vyuo walivyoanza kupata misukosuko kila walipoikosoa Serikali ya Rais Daniel arap Moi.

Katika matoleo yaliyopita tuliangalia namna baadhi ya wanasiasa wa Kenya, wanafunzi wa elimu ya juu na wahadhiri wa vyuo walivyoanza kupata misukosuko kila walipoikosoa Serikali ya Rais Daniel arap Moi.


Rais Moi alianza kuwaandama wapinzani wake, baadhi yao wakiwekwa kizuizini na wengine kukabiliwa na mashtaka mbalimbali. Wanasiasa wengine wakosoaji walipoona hali inazidi kuwa mbaya, walilazimika kuikimbia nchi.

Kukiwa na migogoro ya kisiasa iliyoikumba Serikali ya Rais Moi, kwa upande wa jeshini kulikuwa na tatizo jingine lililokuwa likiongezeka kila siku. Wanajeshi wengi wa vyeo vya chini walikuwa katika hali ya kunung’unika kila mara. Mambo haya na mengine yalifanya mapinduzi yatarajiwe.

Maadili na nidhamu ndani ya Jeshi la Anga la Kenya (KAF) yalikuwa yakishuka kutokana na hasira iliyosababishwa na huduma duni jeshini kama uhaba wa nyumba za kuishi askari, ukosefu wa sare, chakula duni na uhusiano mbaya kati ya wanajeshi wa vyeo vya chini na maofisa wakuu.

Majadiliano miongoni mwa maofisa wa KAF waliokata tamaa yalianza. Sehemu kubwa ya majadiliano hayo ni namna ya kupata hali bora wawapo kazini.

Hata hivyo, uwezekano wa kufanyika mapinduzi ulianza mapema mwaka 1979. Ofisa mmoja wa KAF aliyeitwa James Dianga alikamatwa, akashtakiwa katika mahakama ya kijeshi na kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya uchochezi. Alianza kutumikia adhabu hiyo mwaka 1981.

Dianga alikuwa ameanza kukusanya idadi fulani ya wanajeshi kutoka Jeshi la Anga la Kenya ambao, kama alivyokuwa yeye, hawakuwa wameridhishwa na hali ya maisha makambini mwao. Lengo la kuwakusanya ilikuwa ni kuwashawishi waone uwezekano wa kufanya mapinduzi. Ingawa awali ilisemwa kuwa huo ni uvumi, baadaye alikamatwa, akashtakiwa na mahakama ya kijeshi na baadaye kuhukumiwa kifungo.

Uvumi mwingine wa njama ulidhihirika mwaka 1981, wakati zilipofunguliwa kesi mbili tofauti za uhaini zilizowahusu Andrew Mungai Muthemba na Dickson Kamau Muiruri. Hawa wawili walishtakiwa kwa kujaribu kuunda kikosi cha mauaji cha maofisa wa kijeshi ili kumuua Rais Moi.

Kilichojulikana wakati huo ni kwamba kati ya Desemba 15, 1980 na Februari 23, 1981, Muthemba—ambaye ni binamu wa aliyekuwa Waziri wa Katiba wa Kenya, Charles Njonjo, alimshawishi mwanajeshi mmoja aliyeitwa Koplo Joseph Shimba kuiba mabomu 10 ya kurusha kwa mkono, idadi isiyojulikana ya mabomu ya ndege na silaha nyingine.

Alhamisi, Machi 19, 1981, Wakenya ambao hawakujua habari za kuwapo kwa njama za kuipindua Serikali ya Rais Moi waliamka na kupata habari kwamba mfanyabiashara wa Nairobi, Andrew Mungai Muthemba alishtakiwa kwa kujaribu kupindua Serikali kwa njia zisizo halali.

Kesi ya Muthemba ilijiri wakati ambapo Moi alikuwa akipata wasiwasi kuhusu njama za kumwondoa madarakani.

Aprili 1980, Rais Moi alikuwa amewaonya wapinzani wake na wale “waroho wa madaraka” kwamba angewafunga ikiwa hawataitii Serikali yake.

Ni katika mkanganyiko huo wa kisiasa ambapo mwanasheria mkuu wakati huo, James Karugu na aliyekuwa mwendesha mashtaka mkuu wa umma, Sharad Rao walipata uteuzi wa haraka.

Katika ushahidi uliotolewa mahakamani, ilidaiwa kuwa alimshawishi Kapteni Ricky Waithaka Gitucha kuiba maguruneti 100, mizinga, bunduki na risasi, vilipuzi vya plastiki na silaha nyingine mbalimbali.

Ingawa kesi ya Muthemba na Muiruri ilihusishwa na jitihada za kumvunjia heshima Njonjo, James Dianga alikuwa sehemu ya njama iliyofikia kilele Agosti 1, 1982.

Kukamatwa kwake, kushtakiwa na baadaye kuhukumiwa kuliharibu mipango ya mapinduzi. Lakini majadiliano ya mapinduzi yalianza tena Machi 1982. Safari hii vikao viliongozwa na Private Hezekiah Ochuka Rabala, rafiki wa zamani wa Dianga.

Wakiwa katika kambi ya jeshi ya KAF iliyoko Eastleigh jijini Nairobi, wapanga njama hao waliwasiliana na Mzee Jaramogi Oginga Odinga. Mwanasiasa muhimu zaidi alikuwa mlinzi mkuu wa Odinga aliyeitwa John Odongo Langi, ambaye alikuwa amepata mafunzo ya kijeshi nchini Czechoslovakia.

Dianga ndiye aliyemshawishi Ochuka kujiunga na kikosi hicho cha mapinduzi tangu mwaka 1981, lakini kwa vile yeye mwenyewe alikamatwa Januari 15, mwaka uliofuata, yaani 1982, Ochuka akaendeleza kuanzia hapo, ingawa haikugundulika kuwa walikuwa wakishirikiana naye.

Mahakama ya kijeshi ilipohitimisha kwamba kwa kuwa washirika wa Dianga hawakuweza kupatikana, na kwa vile haiwezekani kwa mtu mmoja kupindua Serikali, Dianga alitiwa hatiani kwa “kufanya uchochezi.”

Alipopatikana na hatia ya kufanya uchochezi alifungwa jela miaka mitatu huko Kamiti.

Huku nyuma ndoto ya kufanya mapinduzi haikufa wala haikufifia. Ndipo Ochuka alichukua usukani Machi 1982 na kusajili wanachama wa Baraza la Ukombozi la Watu (PRC), wengi wao kutoka katika kambi za Jeshi la Anga Nairobi na Nanyuki, yeye akiwa mwenyekiti. John Odongo Langi kazi yake ingekuwa ni kusimamia masuala ya usafiri na vifaa.

Langi alikuwa mmoja wa wanafunzi wengi waliopelekwa Ulaya Mashariki kwa mafunzo ya kijeshi mwanzoni mwa miaka ya 1960. Lakini aliporejea nyumbani hakuajiriwa jeshini. Vile vile, Opwapo Ogai, ambaye alikuwa amepelekwa Kazakhstan baada ya kutumika katika Jeshi la Kenya, naye alikuwa miongoni mwa wapanga njama za mapinduzi

Mtoto wa Jaramogi Odinga, Raila, pia alijiunga na njama hizo. Kazi yake ilikuwa ni kusimamia mapinduzi, kuanzisha kituo kwenye Barabara ya Ngong siku ya mapinduzi hayo. Katika ukurasa wa 215 wa kitabu ‘9/11, Stealth Jihad and Obama’ cha Rohini Desilva kinasema: “Raila Odinga alijaribu kufanya mapinduzi lakini akashindwa”.

Kwa mujibu wa Macharia Munene katika kitabu chake, ‘Historical Reflections on Kenya: Intellectual Adventurism, Politics & International Relations’, Raila Odinga alitoa hata gari lake litumike kuwasafirisha wanajeshi walioasi.

Kati ya Aprili na mwishoni mwa Julai, wapanga njama ambao wengi walikuwa ni Wajaluo, waliiweka mipango yao katika vikao vyao vya majadiliano.

Ingawa kupanga tarehe maalumu ya mapinduzi lilikuwa ni jambo la baadaye, ilionekana kuwa Jumapili ni siku yenye shughuli chache zaidi ikilinganishwa na siku nyingine, na hivyo kusingekuwa na maafa makubwa kwa binadamu ikiwa mapinduzi yangefanyika siku hiyo.

Uvumi kwamba Wakikuyu walikuwa wakipanga njama za kumpindua Moi na kumsimika Kibaki uliwalazimisha waliopanga njama hizo kuharakisha tarehe ya mapinduzi hadi Agosti 1, 1982.

Nini hasa kilitendeka kati ya Machi 1982 tangu Hezekiah Ochuka alipochukua uongozi kutoka kwa James Dianga na Agosti 1, 1982 yalipofanyika mapinduzi? Ni kwa nini Serikali haikuzigundua njama hizo kabla hazijaanza kutekelezwa?


Tukutane toleo lijalo.