Maporomoko ya ardhi yaua watu 10

Raia wakiwa wamekusanyika baada ya vifo vya wanafamilia wao kufuatia mvua iliyoharibu majengo katika kijiji cha Nyamukubi, eneo la Kalehe katika jimbo la Kivu Kusini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mei 6, 2023.

Muktasari:

  • Maporomoko ya ardhi yamesababisha vifo vya watu 10 Mashariki mwa Kongo kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini humo.

Kongo. Watu kumi wamefariki katika maporomoko ya ardhi eneo la Lubero mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo usiku wa kuamkia leo, mamlaka ya eneo hilo imesema maporomoko hayo yanafuatia mvua kubwa za hivi majuzi ambazo zimesababisha mafuriko na kuua mamia ya watu.

Kwa mujibu wa Reuters mvua nyingine iliyonyesha ilishusha kipande cha ardhi katika mlima eneo la Vuveyi Lac, na kuwafunika waathiriwa walipokuwa wamelala katika nyumba zao, amesema Alain Kiwewa, msimamizi wa kijeshi wa Lubero.

"Hadi sasa maiti bado ziko chini, kazi ya kuzitoa inaendelea," amesema Kiwewa.

Wakati huo huo uhaba wa vifaa umedhoofisha juhudi za kuipata miili mingi ambayo bado imefunikwa katika eneo la Kalehe katika jimbo jirani la Kivu Kusini, ambako mafuriko yalikumba vijiji viwili Alhamisi iliyopita, na kuzamisha majengo katika udongo na vifusi.

Kwa mujibu wa Desire Machumu, Mkuu wa Msalaba Mwekundu Kivu Kusini, hadi jumatano asubuhi, idadi ya waliofariki kutokana na mafuriko ya Kalehe imefikia 426 huku takribani watu 1,000 wakiwa bado hawajapatikana.

Wafanyakazi wa misaada wanatarajia kukaa katika eneo la mbali la milimani kwa wiki kadhaa huku uwezekano wa mlipuko wa kipindupindu ukitazamiwa, kutokana na ukosefu wa vyoo, amesema Machumu.

Mvua zinazoendelea nchini humo kuongezeka kwa kiwango cha maji katika baadhi ya maeneo na kuongeza uwezekano wa mafuriko, alisema mhandisi wa hali ya hewa na haidrojeni Theodore Ilemba.

Pia mvua ilisababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi katika nchi jirani ya Rwanda wiki iliyopita, na kuua watu 130 huku ikiharibu nyumba zaidi ya 5,000.