NMB yasaidia walioathirika na mafuriko Mtwara

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Hanafi Msabaha akizungumza leo katika Kijiji cha Kivava kilichokumbwa na mafuriko. Picha na  Mwanamkasi Jumbe

Mtwara. Benki ya NMB imetoa msaada wa magodoro, mashuka na vifaa vya shuleni vyenye thamani ya Sh5 milioni kwa Kaya zilizoathirika na mafuriko wilayani Mtwara.

Akizungumza katika Kijiji cha Kivava kilichopo Kata ya Mahurunga, kwa niaba ya Meneja wa NMB Kanda ya Kusini Agustino Bayona amesema kuwa benki hiyo imetoa magodoro 80, mashuka 80, katoni 6 za madaftari na moja ya kalamu vyote vikiwa na thamani ya Sh5 milioni.

"Tumesikitishwa sana na mafuriko yaliyotokea sisi NMB tumeguswa na majanga haya na kuonelea kushirikiana na wilaya kupitia kitengo chetu cha kurudisha kwa jamii, (CSR) kwa kutoa sehemu ya faida yetu ya mwaka

 uliopita" amesema Bayona.

Amesema NMB inatambua kuwa shule zimefunguliwa na kuna wanafunzi waliopoteza vifaa vya shule hivyo imetoa vifaa vya shule ili watoto wasisimame masomo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kivava, Hamisi Chihelo amesema kuwa mafuriko hayo yaliyotokea mwanzoni mwa mwezi huu wa April, 2023 yameathiri Kata nzima ya Mahurunga yenye wananchi zaidi ya 14000 ambao wengi wanategemea kilimo cha mpunga na mahindi mabondeni ambako ndiko mafuriko yametokea na kusomba mashamba yote.

Diwani wa Kata ya Mahurunga, Selemani Ally Nampanye ameishukuru benki ya NMB kwa msaada na kuongeza kuwa benki hiyo imekua mdau mkubwa wa maendeleo katika kata hiyo kupitia sera yake ya kurudisha kwa jamii.

Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Hanafi Msabaha ameishukuru benki ya NMB kwa kuwashika mkono.

"Tunashukuru kwa kutushika mkono na mchango wenu tunauthamini, tutauenzi, serikali inafanya kazi na wadau ambao tunawategemea sana hususan kipindi cha majanga kama hichi" amesema Msabaha.