Marekani yamuwekea vikwazo Rais Mnangagwa

Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa.

Muktasari:

  • Jana Jumatatu Rais Joe Biden alitia saini agizo la kusitisha dharura ya kitaifa ya Zimbabwe na kubatilisha vikwazo mahususi vya Zimbabwe.


Washington. Serikali ya Marekani imetangaza kuwawekea vikwazo Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, mkewe Auxillia Mnangagwa, Makamu wa Rais Constantino Chiwenga na maofisa wengine waandamizi wanane.

Vikwazo hivyo vimetangazwa leo Jumanne Machi 5 2024 na idara ya Serikali  ya Marekani inayohusika na udhibiti wa mali za kigeni ikiwashutumu Rais Mnangagwa, mkewe Auxillia, Makamu wa Rais Chiwenga, maofisa nane wa Serikali mashirika matatu kwa kuhusika na  ufisadi na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu ya Marekani, vikwazo hivyo vipya vinawalenga viongozi wakuu kwa kuzuia mali zao nchini Marekani ikiwamo kuwazuia kusafiri kwenda Marekani.

 Vikwazo hivyo vipya vinachukua nafasi ya mpango mpana ulioanzishwa miongo miwili iliyopita.

"Tunaendelea kushuhudia ukiukwaji mkubwa wa haki za kisiasa, kiuchumi na kibinadamu," imesema taarifa ya Ikulu ya White House.

Auxillia Mnangagwa, mke wa Rais wa Zimbabwe.

 "Kulengwa kwa mashirika ya kiraia na vikwazo vikali vya shughuli za kisiasa vimeminya uhuru wa kimsingi, wakati wahusika wakuu, wakiwemo viongozi wa Serikali, wamefuja rasilimali za umma kwa manufaa yao kibinafsi.

"Shughuli hizi haramu zinasaidia na kuchangia mtandao wa uhalifu wa kimataifa wa rushwa, magendo na utakatishaji wa fedha unaofanya umaskini kuongezeka kwenye jamii nchini Zimbabwe, kusini mwa Afrika na sehemu nyingine za dunia."

Hii ni mara nyingine kwa Zimbabwe kuwekewa vikwazo, mwanzoni mwa miaka ya 2000 nchi hiyo ilipoanza kutekeleza mpango wa mageuzi ya ardhi na kutoza ardhi kutoka kwa wakulima wazungu wachache ili kuzigawanya upya kwa Wazimbabwe wasio na ardhi, nchi hiyo iliwekewa vikwazo vya kiuchumi.

Pia, Mnangagwa anatuhumiwa kuwalinda wasafirishaji wa dhahabu na almasi wanaoendesha shughuli zao nchini Zimbabwe, kuwaelekeza maofisa wa Serikali kuwezesha uuzaji wa dhahabu na almasi katika masoko haramu na kuchukua hongo ili kupata huduma zake.

Makamu wa Rais wa Zimbabwe, Constantino Chiwenga.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Anthony Blinken amesema vikwazo hivyo ni sehemu ya sera mpya ya vikwazo dhidi ya Zimbabwe ambayo Marekani inatekeleza kufuatia Rais Joe Biden kuidhinisha amri mpya ya utendaji ya vikwazo kwa Zimbabwe ambao ulianza kutumika tangu mwaka 2003.

Pia, jana Jumatatu Rais Joe Biden alitia saini agizo la kusitisha dharura ya kitaifa ya Zimbabwe na kubatilisha vikwazo mahususi vya Zimbabwe.

Sasa, utawala unatumia agizo kuu la enzi ya Rais Donald Trump linalotekeleza Sheria ya Uwajibikaji ya Haki za Kibinadamu ya Global Magnitsky kama mamlaka yake ya kutoa vikwazo.

Ikulu ya White House inasema katika taarifa yake kwamba: "Vikwazo kwa watu hawa na mashirika haviwakilishi vikwazo kwa Zimbabwe au umma wake. Utawala unasisitiza dhamira yake ya kufanya kazi na watu wa Zimbabwe; itaendelea kuunga mkono kwa dhati mashirika ya kiraia, watetezi wa haki za binadamu na vyombo vya habari huru ili kukuza maadili yanayowiana na Sheria ya Demokrasia na Ufufuo wa kiuchumi wa Zimbabwe ya 2001.

“Kuchukua hatua za ziada kuwawajibisha wale wanaowanyima Wazimbabwe uhuru wa kidemokrasia na utawala bora wanaostahili,” inasema taarifa hiyo.

Chini ya mpango huo mpya, Wazimbabwe waliokuwa chini ya vikwazo vya Marekani vya enzi ya Rais Robert Mugabe wataona vikwazo vimeondolewa.

Mwaka wa 2022, Marekani iliwawekea vikwazo watoto wa kiume wa Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa.

“Mabadiliko tunayofanya yanalenga kuweka wazi kile ambacho kimekuwa kweli siku zote: vikwazo vyetu havikusudiwi kuwalenga watu wa Zimbabwe.

“Tunaelekeza upya vikwazo vyetu kwenye malengo ya wazi na mahususi, mtandao wa uhalifu wa Rais Mnangagwa wa maofisa wa Serikali na wafanyabiashara ambao wanahusika zaidi na ufisadi au ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya watu wa Zimbabwe," amesema Naibu Katibu wa Hazina wa Marekani Wally Adeyemo.

Mnangagwa anatuhumiwa kuwalinda wasafirishaji wa dhahabu na almasi wanaofanya kazi nchini Zimbabwe na kuwaelekeza maafisa wa Serikali kuwezesha uuzaji wa dhahabu na almasi katika masoko haramu na kuchukua hongo ili kupata huduma zake.

Uchunguzi wa Al Jazeera mwaka jana uligundua kuwa Serikali ya Zimbabwe ilikuwa ikitumia magenge ya magendo kuuza dhahabu yenye thamani ya mamia ya mamilioni ya dola, na hivyo kusaidia kupunguza athari za vikwazo. Dhahabu ni mauzo makubwa zaidi ya nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken amesema hatua hizo mpya ni sehemu ya sera yenye nguvu zaidi na inayolengwa zaidi ya vikwazo kwa Zimbabwe na alionyesha wasiwasi wake juu ya kesi kubwa za rushwa na ukiukaji wa haki za binadamu.

"Viongozi wakuu, ikiwa ni pamoja na maofisa wengine wa Serikali ya Zimbabwe, wanawajibika kwa vitendo hivi, ikiwa ni pamoja na uporaji wa hazina ya Serikali ambayo inawaibia Wazimbabwe rasilimali za umma," amesema Blinken katika taarifa yake na kungeza kuwa: "Kesi nyingi za utekaji nyara, unyanyasaji wa kimwili na mauaji kinyume cha sheria zimewaacha wananchi wakiishi kwa hofu."

Hata hivyo, msemaji wa Serikali ya Zimbabwe, Nick Mangwana kwenye akaunti ya X ameandika: "Hilo lilisemwa kwa muda mrefu Rais wetu yuko chini ya vikwazo, Zimbabwe inabakia chini ya vikwazo visivyo halali, maadamu wanachama wa familia ya kwanza wako chini ya vikwazo, Zimbabwe inabakia chini ya vikwazo visivyo halali, na mradi uongozi wa juu uko chini ya vikwazo, sote tuko chini ya vikwazo.”

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Marekani, Matthew Miller alijibu kwa mzaha: "Ni nadra kuona Serikali ikisema kuwa vikwazo kwa Rais aliyeketi ni ushindi kwa Serikali."

Mnangagwa, ambaye chama chake cha Zanu-PF kilichoanzishwa Agosti 8, 1963 kimekuwa madarakani kwa zaidi ya miongo minne, alitangazwa mshindi katika uchaguzi wa Agosti mwaka jana ambao waangalizi wa kimataifa walisema uchaguzi huo ulipungukiwa na viwango vya kidemokrasia.

Mnangagwa aliingiia madarakani baada ya kuchukua nafasi kutoka kwa Rais Robert Mugabe mwaka 2017. Mugabe aliyefariki dunia miaka miwili baadaye akiwa na umri wa miaka 95.

(Imeandikwa na Noor Shija)