Mbaroni kwa kukutwa na mabaki ya maiti ya kichanga

Muktasari:

  • Mwanaume mmoja nchini Zambia amekamatwa na polisi baada ya kukutwa na mabaki ya maiti ya kichanga kilichozikwa mwezi uliopita.

Zambia. Polisi katika wilaya ya Kalabo iliyopo jimbo la Magharibi mwa Zambia wanamshikilia mwanaume mwenye umri wa miaka 42 kwa kosa la kukutwa na mwili wa mtoto uliofukuliwa huku ukihifadhi kwenye gunia.

Inaripotiwa kuwa mtoto huyo wa kike alifariki akiwa na umri wa miezi mitatu na akazikwa Aprili 10, 2023. Tovuti ya Zambian Observer ya nchini humo imeripoti.

Babu wa marehemu huyo amesema tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Nalusheke eneo la Lyahonga ambapo mabaki ya mtoto huyo yalikutwa yakiwa yamefungwa kwenye gunia huku baadhi ya viungo vya mwili vikiwa vimekatwakatwa.

Anasema watoto waliokuwa wakiokota matunda pori walikuta mabaki ya mtoto huyo karibu na kijiji na wananchi walifanikiwa kufuatilia nyayo hizo ambazo ziliwafikisha hadi alipokuwa mtuhumiwa.

Naye Afisa Mfawidhi wa Polisi Kalabo, Humphrey Banda, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba upelelezi umeanza ili kupata undani wa tukio hilo la kihalifu.

Mabaki ya mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Wilaya ya Kalabo ukisubiri kufanyiwa uchunguzi na kuzikwa upya.