Mbaroni kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake
Muktasari:
- Mauaji hayo yanadaiwa kuripotiwa na kaka wa marehemu kuwa mwili wa dada yake ulichinjwa na kutupwa kando ya barabara ya kijiji cha Luwayo na mpenzi ambaye alizaa naye mtoto. Marehemu alikatwa sehemu mbili, kichwa na sehemu nyingine, na kwamba washukiwa wawili wametiwa mbaroni.
Uganda. Wakazi wa Kijiji cha Luwayo, Wilaya Buikwe nchini Uganda, wamebaki na mshangao mkubwa baada ya mwanaume kudaiwa kamtakata mpenzi wake ambaye ni mama wa mtoto wake hadi kufa.
Msemaji wa Polisi Mkoa wa Ssezibwa Hellen Butoto amesema uchunguzi kuhusiana na tukio hilo umeanza ilia kubaini sababu za mauaji ya Priscilla Agasiru yanayodaiwa kufanywa na mpenzi wake.
Kwa mujibu wa msemaji huyo, Ekurius Wazemba na babake, ambao ni wakazi wa eneo hilo, wamekamatwa kwa madai ya kuhusishwa na mauaji hayo ambayo yametokea Julai 11 katika kijiji cha Luwayo.
“Suala hilo liliripotiwa na kaka wa marehemu kuwa mwili wa dada yake ulichinjwa na kutupwa kando ya barabara ya kijiji cha Luwayo na mpenzi ambaye alizaa naye mtoto. Marehemu alikatwa sehemu mbili, kichwa na sehemu nyingine. Tuna washukiwa chini ya ulinzi wetu wa polisi ambao wanatusaidia katika uchunguzi,” Butoto amesema.
Maafisa wa eneo la uhalifu (SOCO) na wapelelezi wa mauaji wametembelea eneo la tukio kukusanya ushahidi huku uchunguzi ukiendelea. Wamepata viatu vya bluu na panga kwenye eneo la uhalifu, ambapo dalili za mapambano zilionekana.
Mwili huo umehamishiwa katika Hospitali Kuu ya Kawolo kwa uchunguzi wa kitabibu, huku uchunguzi wa chanzo cha kifo hicho ukiendelea.
Kulingana na ripoti ya polisi juu ya uhalifu ya 2022, matukio ya mauaji yanayotokana na unyanyasaji wa majumbani yalikuwa yamepungua kwa aslimia 19.9 na kwamba jumla ya kesi 301 ziliripotiwa ikilinganishwa na kesi 376 zilizoripotiwa 2021.
Ripoti hiyo hiyo inaangazia ongezeko la aslimia 3.3 la kesi za mauaji nchini kote, na jumla ya kesi 4,043 ziliripotiwa polisi kufikia mwisho wa 2022, ikilinganishwa na kesi 3,912 mnamo 2021.