Mgogoro wa malezi ulivyosababisha vifo vya watu sita
Muktasari:
- Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Ujerumani, waliofariki ni wanawake wanne na wanaume wawili, huku watu wengine kadhaa wakijeruhiwa
Ujerumani. Watu sita wameuawa kwa kupigwa risasi katika kituo cha ustawi wa watoto katika mji wa Stade, kaskazini mwa Ujerumani.
Kwa mujibu wa tovuti ya CNN tukio hilo limetokea jana Jumatatu Juni 29, 2026 saa 12:10 jioni kwa saa za eneo hilo, katika kituo hicho kilichopo mtaa wa Dankerstrasse.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi nchini humo, waliofariki ni wanawake wanne na wanaume wawili, ambao wote walikuwa wafanyakazi wa kituo hicho.
Taarifa hiyo inafafanua watu watano walifariki dunia hapohapo na mmoja alifariki hospitali alipokuwa akipatiwa matibabu ya majeraha aliyoyapata kwenye shambulio hilo.
Pia watu kadhaa wamejeruhiwa japokuwa taarifa hiyo haijatoa idadi kamili ya majeruhi.
Vilevile inaeleza uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa malezi ya mtoto.
Taarifa hiyo ya Polisi inaeleza mtoto wa kike mwenye umri wa miezi mitatu pamoja na mama yake walikuwa ndani ya ofisi wakati wa shambulio, lakini hawakupata madhara yoyote.
Polisi wamewakamata watu watatu, akiwemo mshukiwa mkuu wa tukio hilo na kuthibitisha hakuna tishio lolote linaloendelea kwa wananchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jimbo la Lower Saxony, Daniela Behrens amesema uchunguzi wa awali unaonyesha shambulio hilo lilihusishwa na mgogoro wa kifamilia.
Mkuu wa Polisi wa Lueneburg, Kathrin Schuol, amesema mtuhumiwa ni mwanaume mwenye umri wa miaka 45, raia wa Uturuki aliyezaliwa Ujerumani na anayeishi Hanover.
Schuol amesema mwanaume huyo alikuwa na miadi katika kituo hicho Jumatatu kwa ajili ya mazungumzo kuhusu haki ya malezi ya binti yake, ambapo alikutana na baadhi ya waathirika kabla ya shambulio kutokea.
Baada ya kutekeleza shambulio hilo, mshukiwa alikimbia eneo la tukio kwa kutumia gari lililoendeshwa na mwanamke.
Polisi wanaendelea na uchunguzi kubaini mazingira kamili ya tukio hilo huku wakiamini mgogoro wa malezi ya mtoto ndiyo chanzo kikuu cha shambulio hilo.