Mgonjwa aiba ambulance iliyombeba kumuwahisha hospitali

Muktasari:

  • Mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 47, alikuwa amepelekwa na gari hilo katika Hospitali ya Manhattan kwa matibabu, baada ya kufika hospitali, alitoroka kisha kwenda kuliiba na kutokomea nalo hadi pale Polisi walipolifuatilia gari hilo kupitia GPS na kumkamata.

New York. Matthew Checko (47) amechukua nafasi katika vichwa vya habari nchini Marekani baada ya kuamua kuiba gari ya wagonjwa (Ambulance) iliyokuwa imempeleka katika hosptitali iitwayo ‘Mlima Sinai Morningside’ iliyoko Manhattan kwa ajili ya matibabu.

Tovuti ya Daily News ya nchini humo imesema baada ya Checko kufikishwa hospitalini hapo alitoka kinyemera kisha kuliiba gari hilo lililokuwa limeegeshwa na funguo zikiwa ndani kisha kutokomea nalo.

Taarifa ya Polisi imeeleza tukio hilo lilitokea siku ya Alhamisi, Machi 30 ambapo gari hilo lilikuwa limeegeshwa nje ya hospitali na halikuwa limefungwa wala hakukuwa na mtu ndani ambapo Checko alitoroka hospitalini saa kumi na moja alfajiri.

Checko alifanikiwa kuingia ndani ya gari hilo akaliendesha umbali wa kilomita zaidi ya 40, wakati polisi walipolifuatilia kupitia GPS, kisha walijaribu kumsimamisha na kulizuia lakini aliwapuuza kwa kupita na mwendao wa kasi.

Polisi waliamua kuweka kifaa ambacho kilitoboa magurudumu ya ambulensi hiyo na alikamatwa kwa makosa ya ulaghai, kumiliki mali ya wizi, kutoroka afisa wa polisi na kuendesha gari akiwa amelewa.

Imeandaliwa na Sute Kamwelwe