Mtaliano aliyebaka mabinti 160 anaswa

Muktasari:

Raia wa Italia amekamatwa nchini Ufaransa kwa kibali kilichotolewa na Ujerumani, ambako anasakwa kwa makosa 160 ya kubaka na mashambulizi ya kingono dhidi ya binti yake na watoto wengine, polisi imeiambia  AFP leo Ijumaa.

Paris, Ufaransa . Raia wa Italia amekamatwa nchini Ufaransa kwa kibali kilichotolewa na Ujerumani, ambako anasakwa kwa makosa 160 ya kubaka na mashambulizi ya kingono dhidi ya binti yake na watoto wengine, polisi imeiambia  AFP leo Ijumaa.

Mtu huyo mwenye umri wa miaka 52 alikamatwa Ijumaa iliyopita kusini mwa Strasbourg, karibu na mpaka wa Ufaransa akituhumiwa kufanya makosa hayo katika kipindi cha miaka 14 kuanzia mwaka 2000.

Ujerumani ina uchunguzi wa mashauri 122 yanayochunguzwa dhidi yake, kilisema kitengo kinachoshughulikia makosa hayo cha BNRF.

Mtaliano huyo anatuhumiwa kumbaka binti yake kwa karibu miaka 10 kuanzia mwaka 2000. Anatuhumiwa kufanya kosa kama hilo na kwa kipindi hicho, dhidi ya mabinti wadogo wa marafiki tofauti.

"Alifanya vitendo hivyo ndani ya familia," ilisema BNRF.

Polisi wa Ujerumani waliiarifu BNRF mapema mwezi Oktoba kuwa mtu huyo aliyekuwa akisakwa alitoroka Ujerumani na kwenda Alsace mashariki mwa Ufaransa.

Alikamatwa akiwa nyumbani kwa mpenzi wake mjini Rumersheim-Le-Haut, kusini mwa Strasbourg na amewekwa katika gereza la Colmar lililo karibu na eneo hilo akisubiri kusafirishwa kwenda Ujerumani.