Ukosefu wa takwimu unavyoathiri sekta ya uvuvi nchini

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Riziki Shemdoe akizungumza wakati akifungua mafunzo ya utayarishaji takwimu za samaki.

Muktasari:

  • Samaki kwenye maziwa na habari  wanaweza kuvuliwa hadi wakaisha kutokana na kutokuwa na mipango ya takwimu

Dar es Salaam.  Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Profesa Riziki Shemdoe amesema Tanzania ina upungufu takwimu za samaki kwenye maziwa na bahari huku akitaja faida ya uwepo wake ni kusaidia uendelevu wa rasilimali hizo.

Profesa Shemdoe amesema kukosekana kwa takwimu hizo, samaki kwenye vyanzo hivyo wanaweza kuvuliwa hadi wakaisha kutokana na kutokuwa na mipango.

Hata hivyo, amesema athari nyingine ni Tanzania kushindwa kujenga hoja kimataifa kupewa eneo kubwa kwa ajili ya uvuvi kutokana na kukosa takwimu za samaki waliopo.

Profesa Shemdoe ameeleza  hayo jana Aprili 29,2024  wakati akifungua wa mafunzo ya siku tatu ya namna ya utayarishaji wa takwimu za samaki walipo nchini kwenye bahari na maziwa ukihusisha  wataalamu wa Tanzania, Zambia, Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Burundi.

Mafunzo hayo yanatolewa na Shirika la Chakula Duniani la Umoja wa Mataifa (FAO) yakifadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Ujerumani kwa nchi za Afrika Karibia na Pasifiki.

“Tumekuwa na changamoto, tuna upungufu wa taarifa ya kiasi gani cha samaki tuliyonayo kwenye maziwa na bahari, hivyo mafunzo haya ni muhimu kwa wataalamu wetu kujaribu kupata njia  nzuri ya kupata takwimu hizi, kazi hii inataka kuanza kufanyika ziwa Tanganyika hivyo tuna wawakilishi wa nchi nne zinazopakana na ziwa hilo,” amesema.

Amesema mafunzo hayo Serikali kwa kushirikiana na FAO pamoja na EU wamewekeza kwa ajili ya kutengeneza wataalamu wa kukusanya taarifa hizo.

Profesa Mdoe amesema uwepo wa takwimu za kutosha zitaisaidia Tanzania kujenga hoja kwa vyombo vya kimataifa.

 “Tunavua samaki wanaitwa jodari, tunapokwenda kwenye mikutano mikubwa tunatengewa kitu kinaitwa kota ni kiasi gani kama Tanzania mnatakiwa kuvua kama hamna takwimu za kutosha mnapojenga hoja ya kugawiwa kiasi kikubwa cha kuvua mnaulizwa takwimu ziko wapi,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uvuvi na Ufugaji wa Samaki wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika Beatrice Marwa amesema mafunzo hayo ni muhimu kuwezesha nchi hizo kuwa na njia moja ya ukusanyaji wa takwimu za samaki.

“Samaki hawana mipaka unayemkuta Congo kesho unaweza kumkuta Zambia, hivyo ni vizuri kuwa na njia moja ya kukusanya takwimu, tayari tumekubaliana njia ya kutumia kwa hiyo mafunzo haya yanakwenda kuwafunza wataalamu wanaokwenda kusimamia wingi wa samaki ziwa Tanganyika,” amesema

Mtaalamu huyo amesema upatikanaji wa takwimu utasaidia kulinda rasilimali za uvuvi ziwa Tanganyika na uhifadhi wa chakula.

Kwa upande wake Mwakilishi wa mradi wa kuendelea uvuvi FISH4ACP kutoka FAO Steven Gocca amesema uwepo wa takwimu za samaki zitasaidia watunga sera kufanya maamuzi yatakayochochea ukuaji wa uchumi kupitia agenda ya uchumi wa buluu.

Mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Congo, Dk Deo Mushagalvsa amesema bila takwimu ni ngumu kulinda rasilimali zilizopo kwenye maziwa na bahari hivyo mafunzo hayo ni muhimu kwa nchi nne zilizo pembezoni mwa Ziwa Tanganyika kulinda rasilimali ndani ya ziwa hilo.