Mwanafunzi apiga risasi watu sita, ajiua

Maofisa wa polisi wakifanya doria katika Shule ya SekondariPerry lilipotokea tukio la ufyatuaji wa risasi, jana Januari 4, 2024
Muktasari:
- Mwanafunzi katika shule moja nchini Marekani amemuua mtu mmoja na kujeruhi wengine watano kwa risasi na kisha kujiua kwa kujifyatulia risasi.
Perry, Iowa. Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Perry iliyopo Jimbo la Lowa nchini Marekani, amemuua mtu mmoja na kujeruhi wengine watano kwa risasi na kisha kujiua kwa kujifyatulia risasi.
Tukio hilo limetokea jana Alhamisi, Januari 4, 2024 ikiwa ni siku ya kwanza ya masomo baada ya mapumziko ya msimu wa baridi, maofisa wa sheria wamesema.
Kwa mujibu wa Reuters, aliyeuawa katika tukio hilo ni mwanafunzi wa kidato cha sita na mtuhumiwa ametambuliwa kama Dylan Butler, wamesema maofisa hao kwenye mkutano na wanahabari.
Mkurugenzi msaidizi wa idara ya upelelezi wa jinai wa jimbo hilo, Mitch Mortvedt amesema wamegundua kilipuzi walipokuwa wakifanya upekuzi shuleni hapo.
Amesema shambulio hilo lilitokea saa 1:30 asubuhi kabla ya wanafunzi na walimu wengi kuingia ndani ya jengo hilo.
Amesema wanne kati ya waliojeruhiwa ni wanafunzi na mwingine ni msimamizi wa shule, alisema Mortvedt, ambaye alikataa kutoa majina.
Wilaya ya Easton Valley, ilitoa taarifa kwamba imepokea habari kuwa Dan Marburger, mkuu wa shule hiyo, ndiye msimamizi aliyepigwa risasi katika shambulio hilo.
Mwathiriwa mmoja alikuwa katika hali mbaya, lakini hakuwa na majeraha makubwa, Mortvedt amesema, huku wengine wanne wakiwa katika hali nzuri.
"Mkasa huu umetikisa jimbo letu na ninataka jumuiya hii ijue kila Iowa inasimama pamoja na waathiriwa," amesema Gavana wa Iowa Kim Reynolds kwenye mkutano huo.
Maofisa wa FBI kutoka ofisi ya Omaha-Des Moines walikuwa wakisaidia katika uchunguzi huo na Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Merrick Garland amefahamishwa kuhusu ufyatuaji huo.
"Hatuwezi kuruhusu majanga haya kuendelea, lazima tufanye kitu," amesema Katibu wa Habari wa Ikulu ya White House, Karine Jean-Pierre.
Mwaka 2023 kulikuwa na matukio 346 yaliyohusisha ufatuaji wa risasi katika maeneo ya shule nchini humo kulingana na tovuti ya kuhifadhi taarifa ya K-12.
Matukio manne kama hayo tayari yamefanyika ndani ya mwaka mpya wa 2024, ikiwa ni siku tano tu tangu mwaka uanze kulingana na tovuti hiyo.