Mwanajeshi aua watu 13 kwenye msiba wa mwanaye

Muktasari:

  • Baada ya kutekeleza mauaji hayo, vikosi vya kijeshi vinavyojumuisha wanajeshi wa DRC tayari vimetumwa kumkamata mwanajeshi huyo aliyekimbia baada ya kufanya mauaji hayo ya kinyama.

Kongo. Mwanajeshi mmoja kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) amewafyatulia risasi na kuwaua wanafamilia na baadhi ya watu 13 kwa kosa la kumzika mwanaye bila uwepo wake.

 Msemaji wa polisi katika jimbo la Ituri, Jules Ngongo amesema shambulio hilo limetokea Jumamosi jioni katika kijiji cha Nyakova kilichopo katika jimbo hilo na kusababisha kifo cha mke wake, wakwe zake pamoja na watoto wake wawili.

“Watoto wengine wanane ni miongoni mwa waliouawa na askari huyo ambaye hakutambulika jina mara moja wakati wa shambulizi hilo,” amesema Ngongo kama alivyonukuliwa na kituo cha televisheni cha Al Jazeera.

Ngongo ameongeza kuwa vikosi vya kijeshi vinavyojumuisha wanajeshi wa DRC tayari vimetumwa kumkamata mwanajeshi huyo aliyekimbia baada ya kufanya mauaji hayo.

“Huwezi kuchukua maisha ya mtu, hiki ni kitendo cha utovu wa nidhamu ambacho kitashughulikiwa na Mahakama,” amesema Ngongo.

Kwa upande wake, kiongozi wa kijiji hicho, Baraka Oscar amesema mwanajeshi huyo alifika nyumbani kwake akitokea kituo chake cha kazi na kuwakuta wanafamilia pamoja na wanakijiji wamekusanyika kwa ajili ya mazishi ya mwanae aliyefariki Alihamisi iliyopita.

“Askari hakupendezwa alipowakuta wanafamilia wakiendelea na mazishi ya mwanae bila idhini yake,” amesema Oscar.