Nabii asiyeona ‘abaka’ ndugu wawili, adai kuwaponya utasa

Nakuru. Mfuasi wa kanisa ‘Legion of Mary’ Jacob Wekesa (66), anayejitambulisha kama ‘Nabii,’ amejikuta katika wakati mgumu baada ya mahakama mjini Nakuru, kumtia hatiani kwa makosa ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono.

Wekesa ambaye ana ulemavu wa macho, amekuwa akidai kuwa na uwezo wa kutambua matatizo ya afya ya uzazi kwa wanawake kupitia macho yake ya kiroho, anatuhumiwa kubaka wasichana wawili ndugu.

Japokuwa amekana mashtaka yake, Mahakama mjini hapa, imekuta na hatia ya kuwabaka mabinti hao toka katika familia ambayo ilikuwa imekaribisha ‘nabii’ huyo ambapo alishii nao kwa muda wa kama wiki moja kabla ya kupatwa madhila hayo.

Mwanaume huyo ambaye hupenda kuvaa mavazi ya mtindo wa ‘kikasisi’ yakiwa na nembo ya msalaba, anapambana kujiokoa kutoka katika kifungo cha muda mrefu iwapo mahakama itashawishiwa na upande wa mashtaka.

Masahibu yake yanasemekana kuanza siku ya mwaka mpya alipozuru nyumbani kwa mmoja wa wafuasi wake, Sarah Atieno mkazi kaunti ndogo ya Njoro, kwa lengo la kuwafanyia maombi binti wawili wa mama huyo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, ni katika kipindi alichokaa na familia hiyo, ndipo mnamo Januari 5, 2023; mzee huyo wa miaka 66 alidaiwa kutenda makosa hayo dhidi wasichana hao wawili, watoto wa Sarah.

Mtandao wa Nation unabaisha kuwa, hati hiyo ya mashtaka imeweka wazi kuwa Wekesa anadaiwa kufanya mapenzi kwa makusudi na wasichana hao kinyume na matakwa yao katika uwanja wa ‘Golf Estate’ huko Njoro, japo anakanusha shtaka hilo.

Akitoa ushahidi mbele ya Mahakama hiyo, mmoja wa waathirika amesema ‘nabii’ huyo alipelekwa nyumbani kwao na mama yake mzazi, huku akidai kuwa ni nabii wa kutoka kanisa la Legion of Mary.

Binti huyo aliendelea kuielezea mahakama kuwa ‘Nabii’ huyo ambaye ni mlemavu wa macho (kipofu), alikaribishwa na kutengewa chumba kilichokuwa jirani na chumba cha wasichana hao.


Macho ya Rohoni

Aidha, saa 11 jioni ya siku husika, mwanamume huyo alimwita chumbani kwake na kumwambia kuwa anaona kwa macho yake ya kiroho kwamba alikuwa na tatizo, na kwamba alikuwa tasa, lakini angemponya.

Msichana huyo ameiambia mahakama kuwa alinasa kwa urahisi kwenye mtego wa mwanamume huyo kwa sababu alikuwa na uvimbe kiunoni, ambao alidhani kuwa unaweza kuwa sababu ya utasa alioelezwa.

"Ilikuwa saa 11 jioni aliponiambia nizime taa, nivue nguo zangu na nirukie kitandani ili aweze kunichua uvimbe kiunoni mwangu huku akinikumbusha kuwa huenda sitaweza kupata mtoto," mwanamke alisema.


Uponyaji ndani ya siku moja

Kwa mujibu wa shahidi huyo, ‘nabii’ Wekesa aliendelea kumshikashika pasipostahili na jambo la pili alilolijua ni kwamba mwanaume huyo alikuwa akifanya naye tendo la ndoa.

“Alinivuta karibu na kabla sijajua tunafanya mapenzi, nilipojaribu kupiga kelele alinionya kuwa nikipiga kelele au kumwambia mtu nitajionea mwenyewe kitakachotokea. Na kwamba sikuwa mwanamke pekee ambaye alikuwa amefanya naye," shahidi alisema.

Baada ya tukio hilo, inadaiwa ‘nabii’ huyo alimwambia avae nguo na kuondoka chumbani humo huku akimhakikishia kuwa atapona baada ya siku moja.

Hata vivyo, alishangaa alipoingia chumbani na kumkuta dada yake analia, na alipomuuliza tatizo ni nini, alimwambia kuwa nabii huyo amemfanyia vilevile.

Wawili hao walikimbizwa hospitalini, ambapo madaktari walithibitisha kuwa walinajisiwa kabla ya kpewa dawa.

Mama wa wasichana hao alisema mshukiwa alimtembelea nyumbani kwake akidai alitaka kuombea familia.

Alisema alimkaribisha na kumpa chumba kimoja cha kukaa. Lakini mnamo Januari 5, binti zake walimwambia kwamba walikuwa wameombewa na ‘nabii,’ na kwamba walikuwa na mashaka dhidi ya kile kilichowapata wakati wa maombi.

Kwa mujibu wa utetezi wa mama huyo, aliwapeleka binti zake hospitali, na kugundua kuwa walikuwa wamebakwa.

Baada ya kesi hiyo kuunguruma toka kufunguliwa kwake, mnamo Mei 8, 2023; mahakama iliamua kwamba mshukiwa alikuwa na kesi ya kujibu na na hivyo usikilizwaji wa utetezi wake ulianza.

Aidha, katika utetezi wake alioutoa Mei 15 mwaka huu, Wekesa amekanusha mashtaka hayo na kudai kwamba ulikuwa ni mtego.

Wekesa ameiambia mahakama kwamba alienda nyumbani kwa mwaliko wa mama huyo aliyemtaka awaombee watoto wake, na kwamba yeye ni ‘Mtumishi’ wa walioitwa, utumishi ambao anadai kuupokea toka kwa Mungu, kuwaombea na kuwaponya watu.

“Haiwezekana kwangu kutekeleza kosa hilo kwa sababu wanawake hao walikuwa wakiondoka asubuhi na kurudi usiku sana,” akasema Wekesa.

Hata hivyo, Hakimu Mkazi Edward Oboge amepanga Juni 6 2023 kuwa ndiyo siku ya hukumu.