Sakata la Shakahola, miili iliyofukuliwa yafika 200

Maofisa na wananchi wakipandisha mwili kwenye gari ya polisi baada ya kufukuliwa katika Kijiji cha Shakahola, Kaunti ya Kilifi nchini Kenya. Picha na NMG.

Muktasari:

  • Idadi ya miili iliyofukuliwa katika msitu wa Shakahola yafikia zaidi ya 200 huku hofu kwa familia zilizopotelewa na wapendwa wao ikizidi kutanda.

Nairobi. Idadi ya waliofukuliwa katika msitu wa Shakahola imefikia 201 baada ya jana Jumamosi Mei 13, Polisi kufukua miili mingine 22 huku kukiwa na hofu ya uwepo wa makaburi mwengine. Tovuti ya CTV News imeripoti.

Kwa mujibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu la nchini humo limesema watu waliotoweka wakihusishwa na mahubiri ya Mchungaji Paul Mackenzie ni zaidi ya 600 hivyo baadhi ya familia zimeingiwa na hofu kubwa wakihofia wapendwa wao huenda walishafariki dunia na kuzikwa.

Hadi sasa mamia ya miili imetolewa kutoka kwenye makaburi ya halaiki yaliyotapakaa katika eneo hilo la hekari 800, lililoko katika kaunti ya pwani ya Kilifi.

Mackenzie, ambaye alikamatwa mwezi uliopita, bado yuko kizuizini. Polisi wanapanga kumshtaki kwa makosa yanayohusiana na ugaidi ingawa anasema alishalifunga kanisa lake tangu 2019 na akahamia kwenye ukulima.

Uchunguzi wa miili zaidi ya 100 wiki iliyopita ulionyesha waathiriwa walikufa kwa njaa, kunyongwa na kukosa hewa.

Mackenzie, mkewe na washukiwa wengine 16 watafikishwa mahakamani mwishoni mwa mwezi huu.

Polisi nchini Kenya wamekuwa wakiwahoji viongozi wengine wa dini ambao mafundisho yao yanaaminika kuwa ya upotoshaji na kinyume na haki za msingi za binadamu akiwemo ‘Yesu wa Tongaren’.