Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

NMG yaeleza kuvamiwa, kufungiwa vyombo vyake vya habari Uganda

Muonekano wa eneo la mapokezi katika ofisi za Daily Monitor zilizopo Namuwongo, Kampala.

Muktasari:

  • Uamuzi wa kufungiwa kwa vyombo hivyo vya habari, ulitokana na maelekezo ya Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo, Jenerali Muhoozi Kainerugaba

Uganda. Mapya yameibuka kuhusu kufungiwa kwa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Kampuni ya Nation Media Group (NMG) nchini Uganda, baada ya kampuni hiyo kueleza, wanajeshi walivamia majengo yake na kukata umeme.

Uamuzi wa kufungiwa kwa vyombo hivyo vya habari, ulitokana na maelekezo ya Mkuu wa Majeshi wa nchi hiyo, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, aliyeandika katika ukurasa wake wa mtandao wa X kuwa vyombo hivyo vimefungiwa.

Katika ujumbe huo, Muhoozi ameandika, “siamini katika uhuru wa habari usio na mipaka,” huku akitangaza NTV Uganda na Daily Monitor vimefungwa Uganda na kusisitiza vyombo vingine vya habari nchini humo vitalazimika kufuata sheria.

Hatua hiyo imezua maswali mapya kuhusu uhuru wa habari nchini humo, huku waandishi, wanaharakati na wadau wa haki za binadamu wakifuatilia na baadhi yao kulaani tukio hilo.

Katika taarifa yake iliyoitoa jana, uongozi wa NMG Uganda, umesema majengo yake yaliyopo Namuwongo na katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kampala Serena yalizingirwa na wanajeshi usiku wa kuamkia Juni 28.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wanajeshi waliwasili katika maeneo hayo saa 1:00 usiku na kusababisha kukatika kwa umeme pamoja na kusimamishwa kwa shughuli za kawaida za uzalishaji na usambazaji wa habari.

"Kampuni yetu itaendelea kuwahudumia wasomaji, watazamaji na wasikilizaji kupitia majukwaa ya kidijitali wakati tukifuatilia maendeleo ya hali hii," inaeleza sehemu ya taarifa ya NMG Uganda.

Daily Monitor nayo iliripoti kuwa wanajeshi wenye silaha walizingira ofisi zake huku wakidhibiti njia za kuingia na kutoka katika eneo hilo.

Mbali na Daily Monitor na NTV Uganda, vyombo vingine vinavyomilikiwa na Nation Media Group ikiwamo Dembe FM, KFM, Spark TV na The East African navyo vimeripotiwa kuathiriwa na hatua hiyo.

Katika ujumbe mwingine uliochapishwa mtandaoni, Muhoozi ameeleza kuwa, haamini katika kile alichokiita uhuru usio na mipaka wa vyombo vya habari na kusisitiza kuwa taasisi za habari nchini Uganda zinapaswa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.

Kauli hizo zimeongeza mjadala kuhusu nafasi ya vyombo vya habari katika jamii na mipaka ya mamlaka ya taasisi za dola katika kusimamia shughuli za habari.

Uganda imekuwa ikikosolewa mara kwa mara na mashirika ya kutetea haki za binadamu kuhusu mazingira ya uhuru wa kujieleza na utendaji wa vyombo vya habari.

Muhoozi ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986. Mara kadhaa amekuwa akivuta hisia za umma kutokana na matamshi yake ya kisiasa na kijeshi kupitia mitandao ya kijamii.

Hadi taarifa hii inaandaliwa, Serikali ya Uganda ilikuwa haijatoa tamko rasmi kuhusu sababu za hatua hiyo wala muda ambao vyombo hivyo vitaendelea kusimamishwa shughuli zake.