Ochuka ateka ndege, akimbilia Tanzania-8

Hezekiah Ochuka akiwa amefungwa pingu baada ya kukamatwa. Picha ndogo ni ndege aliyoteka kukimbilia Tanzania.

Muktasari:

  • Katika toleo lililopita tuliona wanajeshi waasi waliotaka kuipindua Serikali ya Rais Daniel Arap Moi walivyoshambuliwa na vikosi vya usalama.

Katika toleo lililopita tuliona wanajeshi waasi waliotaka kuipindua Serikali ya Rais Daniel Arap Moi walivyoshambuliwa na vikosi vya usalama.

Hezekiah Ochuka alipogundua mpango wake wa kuipindua Serikali ya Moi umeshindwa, aliendelea na ‘mpango B’ yaani kutoroka.

Aliwahadaa wenzake anakwenda Kambi ya Laikipia ya Jeshi la Anga la Kenya (KAF) huko Nanyuki kutafuta msaada. Wenzake walikubali kwa urahisi.

Aliondoka na mmoja wao aliyemwamini zaidi, Pancras Oteyo Okumu. Alipofika Nanyuki alimkuta rubani wa ndege za jeshi, meja Nick ole Leshan, alimteka kwa kumshikia bunduki kichwani na kumlazimisha aingie kwenye ndege aina ya ‘DHC-5 Buffalo’ Number 210 kuelekea Dar es Salaam.

Meja Leshan alikuwa pamoja na meja William Marende, aliyekuwa rubani wa ndege za kivita. Meja Marende hakuwahi kuendesha ndege aina ya ‘Buffalo.’

Meja Leshan alidhani anatakiwa kurusha ndege kumpeleka Ochuka Kambi ya Nanyuki lakini ndege ilipopaa tu angani, Meja Leshan aliamrishwa kuelekea Dar es Salaam.

Safari hiyo ilikuwa na shaka kubwa. Ndege haikuwa na mafuta ya kutosha. Isitoshe, safari yenyewe haikuwa imeidhinishwa na Jeshi la Kenya wala hapakuwa na idhini ya Serikali ya Tanzania kuingia kwenye anga yake.

Ochuka alikuwa amechanganyikiwa sana kutokana na mapinduzi yake kushindwa. Alichowaza tu kwa sasa ni kujiokoa.

Alikuwa akitokwa jasho jingi na alikuwa katika hali ya woga sana kiasi kwamba Meja Leshan alihofia angeweza kufanya lolote hata kuua.

Meja Leshan alihofia ndege ingeweza kutunguliwa na wanajeshi wanaomtii Rais Moi. Hofu ya kuuawa na Ochuka ilimfanya arushe ndege hadi Dar es Salaam, hiyo ilikuwa ndiyo safari yake ya kwanza ndefu zaidi katika maisha yake ya urubani wa ndege za kivita.

Walipovuka mpaka, Meja Leshan aliingiwa na hofu nyingine, mafuta ya ndege yanakaribia kuisha.

Hatari ya ndege kuishiwa mafuta ikiwa angani ilimfanya Leshan azungumze na Ochuka, ambaye wakati huo bado alikuwa amemshikia bunduki kichwani.

“Ondoa bunduki yako kichwani mwangu. Tuna tatizo kubwa zaidi ya hilo,” alimwambia Ochuka.

“Tatizo gani?” Ochuka aliuliza.

“Hatuna mafuta ya kutosha kutufikisha Dar es Salaam.”

Ochuka aliondoa bunduki yake kichwani mwa Leshan, akajiweka sawa kisha akamwambia “Usijali afande, Mungu atatusaidia,” alisema Ochuka. Hata hivyo, Mungu alisaidia kama Ochuka alivyoomba kwa sababu walifika Dar es Salaam salama.

Leshan alikuwa ofisa mwandamizi katika Jeshi la Kenya wakati Ochuka alikuwa wa cheo cha chini kabisa. Kwa hiyo hofu nyingine aliyokuwa nayo Leshan ni namna ambayo angeuambia ulimwengu kuwa hakushiriki maasi hayo na aaminike.

Akiwa angani aliwaza mengi. Iwapo ndege ingeanguka kabla ya kufika Dar es Salaam, familia yake ingesumbuliwa kwa sababu ingeaminika alishiriki mapinduzi hayo ya kumng’oa Rais Moi.

Alihofia familia yake ingewindwa maisha yote na kusulubiwa bila hatia. Alitamani kuuambia ulimwengu kuwa alitekwa. Alijaribu kuwasiliana na Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta ili kuwasilisha ujumbe kuwa ametekwa, lakini hakuweza.

Alijaribu pia kuwasiliana na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam, lakini hakuweza kuwasilisha ujumbe wake huku ameshikiwa mtutu wa bunduki kwenye kichwa chake.

Baadaye alifanikiwa kuwasiliana na ndege nyingine, akapata mawasiliano na ndege ya Scandinavian Airlines System (SAS) iliyokuwa ikitoka Afrika Kusini kuelekea Ulaya.

Alijitambulisha kwa wafanyakazi wa ndege hiyo: “Jina langu ni Nick Leshan wa Jeshi la Anga la Kenya. Kuna mapinduzi Kenya. Nimetekwa nyara na wapangaji njama na ninalazimishwa kwa mtutu wa bunduki. Sina uhusiano wowote na mapinduzi. Sina mafuta ya kutosha kunifikisha Dar es Salaam. Tafadhali sambaza taarifa hizi kwa watu wengi uwezavyo.”

Lakini wafanyakazi wa SAS hawakuweza kuelewa ujumbe wake. Hakukata tamaa. Alijaribu tena mara tatu kuwasiliana na SAS.

Wakati huohuo, alishusha ndege chini kwa matumaini angeweza kukuta barabara au hata njia ya ng’ombe ili atue kwa dharura.

Ingawa kuruka chini chini hakukusaidia sana kuokoa mafuta kidogo aliyobakiwa nayo, kuliwaepusha kuonekana kwenye rada ili wasitunguliwe.

Walipokaribia Dar es Salaam, Leshan alilazimika kuomba kutua kwa dharura kwa vile alikuwa akiruka kwa kutumia matone ya mwisho ya mafuta.

Leshan alisema ndege imebakiwa na mafuta yasiyotosha kuendelea na safari kwa dakika tano zaidi na akatangaza kuwa yuko katika hali ya dharura. Halafu akasema ndani ya ndege alikuwa na mtu aliyekuwa amemshikia bunduku nyuma yake hivyo, yuko hatarini.

Kusikia hivyo, Serikali ya Tanzania iliwaruhusu kutua. Dakika chache baadaye ndege ilitua, Leshan aliyekuwa amechoka kabisa, alizimia baada ya ndege kutua.

Akiwa jijini Dar es Salaam, Ochuka aliomba hifadhi ya kisiasa na kudai alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Ukombozi wa Watu wa Kenya na ndiyo maana amekimbia Kenya kama mkimbizi wa kisiasa kwa sababu maisha yake yalikuwa hatarini.

Lakini mjini Nairobi, Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka, Sharad Rao aliomba hati ya kumkamta Ochuka na wenzake na kurejeshwa Kenya. Hati hiyo ilitolewa na Jaji Abdul Rauf. Hata hivyo, Mahakama ya Tanzania ilikubaliana na Ochuka na kutupilia mbali ombi la Kenya la kuwarejesha ‘wakimbizi’ hao.

Jaji Goodwill Korosso alisema ushahidi ulionyesha wanajeshi hao walikubaliana na mpango wa kukimbilia Tanzania na huenda walikubali wazo hilo baada ya kubaini maisha yao yapo hatarini kutokana na kuvamiwa na majeshi ya Serikali.

“Inawezekana wakuu hao walikubali kuja Tanzania kwa kuhofia usalama wa maisha yao upo hatarini na njia pekee ya kujiokoa kutokana na kuendeleza vikosi vya askari wa miguu kwenye Kambi ya Eastleigh ilikuwa ni kutorokea Tanzania.

Jaji Korosso katika uamuzi wake alisema wakuu wawili wa kijeshi hawakuwa na vyeo kwenye mabega yao vya kuwatofautisha na watumishi wengine.

Ochuka alipewa hifadhi ya kisiasa. Baada ya kushindwa kumrejesha Ochuka, Leshan alirejeshwa Kenya na akaingizwa tena kwenye kikosi kipya cha 82 Air Force cha Jeshi la Kenya. Alikuwa ameambatana na kamishna msaidizi wa polisi, A.M Khan.

Kenya, ndani ya siku mbili tangu mapinduzi yashindwe, karibu jeshi lote la zaidi ya askari 2,000 walikamatwa. Mapinduzi ya 1982 yalimpa Rais Moi fursa ya kuwakamata wale aliowaona kuwa ni wapinzani wake wa kisiasa.

Raila Odinga naye alikamatwa. Misimamo mikali ya wanafunzi wa vyuo vikuu ilidhibitiwa. Chuo Kikuu cha Nairobi na Chuo Kikuu cha Kenyatta vyote vilifungwa.

Wanafunzi walipokuwa wakiondoka kwenye makazi yao, walihojiwa na polisi. Takriban 500 walikamatwa, si kwa tuhuma za kushiriki mapinduzi, bali kwa kushiriki katika uporaji. Wahadhiri ambao kwa muda mrefu walifikiriwa kuwa na itikadi kali za kisiasa walikamatwa.


Nini kiliendelea baada ya hapo? Hakikisha haukosi kusoma tena kesho.