Ofisi za Chama cha Bobi Wine zafungwa

Muktasari:
- Polisi na wanajeshi wa Uganda wamefunga ofisi za Chama cha National Unity Platform (NUP), chama kinachoongozwa na mwanasiasa wa upinzani Bobi Wine.
Uganda. Polisi na wanajeshi wa Uganda wamefunga ofisi za Chama cha National Unity Platform (NUP), chama kinachoongozwa na mwanasiasa wa upinzani Bobi Wine.
"Kuna uwepo mkubwa wa maafisa wa usalama katika ofisi zetu huko Kamwokya, na kwa sasa hatuwezi kuzifikia," chama cha NUP kilisema katika chapisho kwenye mtandao wa X leo Jumatatu.
Kulingana na BBC, Bobi Wine pia amesema maafisa hao walivamia makao makuu ya chama chake na kuwazuia watu kuingia au kutoka nje ya majengo hayo.
Mwanamuziki huyo aliyegeukia siasa alisema kwenye mitandao ya kijamii kwamba kizuizi cha maofisa wa usalama kinalenga kusimamisha hafla ya maombi ambayo NUP ilipanga kufanya katika ofisi yake mjini Kampala leo Jumatatu.
Maombi hayo yalikusudiwa kwa ajili ya marafiki wa chama hicho, waliofariki, kuzuiliwa na kutoweka.
Wiki iliyopita, polisi walimpeleka Bobi Wine hadi nyumbani kwake baada ya kurejea Uganda kutoka Afrika Kusini, wakisema kuwa hatua hiyo ilikuwa ni kumzuia kuandaa maandamano.
Pia waliwazuilia makumi ya wafuasi wa Bobi Wine kwa madai kwamba walichochea vurugu na kupanga maandamano haramu.
Bobi Wine amewakosoa maafisa hao wa usalama kwa hatua hiyo, inayoenda sambamba na siku ya uhuru wa Uganda.