Papa Benedict XVI afariki dunia akiwa na miaka 95

Papa Benedict XVI

Muktasari:

  • Papa Benedict XVI amefariki dunia leo Jumaosi Desemba 31, 2022 akiwa na umri wa miaka 95 katika makazi yake ya ‘Mater Ecclesiae’ huko Vatican.

Dar es Salaam. Jumuiya ya wakristu wakatoloki duniani wamepata pigo baada ya kumpoteza aliyekuwa kiongozi wa kanisa katoliki duniani, Papa Benedict XVI ambaye amefariki leo Jumamosi Desemba 31, 2022 katika makazi yake huko Vatican akiwa na umri wa miaka 95.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Papa ya Holy See Press, Benedict XVI amefariki katika makazi yake katika monasteri ya Mater Ecclesiae ambayo aliichagua kama makazi yake baada ya kujiuzulu mwaka 2013.

Wameeleza katika kipindi cha uhai wake Papa Benedict XVI aliongoza kanisa Katoliki kwa muda usiozidi miaka minane hadi, mwaka 2013, akawa Papa wa kwanza kujiuzulu tangu Gregory XII mwaka 1415.

Papa Benedict XVI amefariki leo ikiwa ni siku chache baada ya Papa Francis kuwaomba waumini wa kanisa hilo kumwombea mtangulizi wake huyo, akisema alikuwa “mgonjwa sana.”

Ingawa Papa huyo wa zamani alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu, taarifa zinasema amekuwa na hali mbaya kwa sababu ya uzee.


Jumatano iliyopita, Papa Francis alitoa wito kwa waumini wake huko Vatican “kusali sala maalum kwa ajili ya Papa Benedict” ambaye alisema alikuwa mgonjwa sana.

Papa Benedict XVI ambaye jina lake halisi ni Joseph Ratzinger, alizaliwa Ujerumani, alichaguliwa kuwa papa mwaka 2005 akiwa na umri wa miaka 78, akawa mmoja wa mapapa wakongwe kuwahi kuchaguliwa.

Wakati wa uongozi wake kama Papa, Kanisa Katoliki lilikabiliwa na kashfa, madai ya kisheria na ripoti rasmi katika miongo kadhaa ya unyanyasaji wa watoto kingono uliodaiwa kufanywa na makasisi.

Mapema mwaka huu Papa huyo wa zamani alikiri kwamba makosa yalikuwa yamefanyika katika kushughulikia kesi za unyanyasaji alipokuwa Askofu Mkuu wa Munich kati ya mwaka 1977 na 1982.