Mwabukusi, Madeleka waitwa tena Kamati ya Mawakili

New Content Item (1)

Muktasari:

  •  Mwanasheria Mkuu wa Serikali alimfikisha Wakili Boniface Mwabukusi mbele ya Kamati ya Maadili ya Mawakili Novemba 2023 kwa madai ya utovu wa nidhamu

Dar es Salaam. Wakati Wakili wa Kujitegemea, Boniface Mwabukusi akiitwa na Kamati ya Maadili ya Mawakili kusikiliza hukumu ya kesi namba 10 ya 2023 aliyofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakili Peter Madeleka naye ameitwa kusikiliza kesi yake.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali alimfikisha Wakili Mwabukusi mbele ya kamati hiyo Novemba 2023 kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Mwabukusi aliyepata umaarufu kwa kauli zake za kupinga mkataba wa uwekezaji na uendelezwaji bandari kwa Kampuni ya Dubai World, anadaiwa kutoa kauli za utovu wa nidhamu alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari.

Moja ya kauli iliyotajwa katika malalamiko hayo ni maneno ya Mwabukusi kwamba, “Spika wa Bunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hawajui walichopitisha bungeni kwamba hata Chifu Mangungo anasingiziwa maana yeye alijua ni mkataba.”

Shauri hilo lililoanza kusikilizwa Novemba 20, 2023 liliingia mushkeli baada ya kutokea mabishano ya kisheria yaliyosababisha Wakili wa Mwabukusi, Mpale Mpoki kufungiwa kwa miezi sita.

Barua ya wito ambayo Mwananchi Digital imeiona iliyosainiwa na katibu wa kamati hiyo, Faraji Ngukah ya Aprili 25, 2024 imemtaka Mwabukusi kufika mbele ya kamati itakayoketi Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi Mei 17, 2024 saa tatu asubuhi.

Barua hiyo imeonya, endapo Mwabukusi hatafika, uamuzi utatolewa bila kuwepo kwake kwa mujibu wa kanuni za nidhamu za mawakili.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kwa upande mwingine kamati hiyo imemwita wakili wa kujitegemea, Peter Madeleka kuhudhuria kesi mbili alizofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

AG, Dk Eliezer Feleshi alimtuhumu Madeleka kwa kukiuka maadili ya kitaaluma.

Barua ya wito wa Madeleka mbele ya kamati hiyo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii Februari 23, 2024 ilieleza kuwa AG aliwasilisha malalamiko dhidi ya wakili huyo kuhusu ukiukaji wa maadili ya kitaalumu.

Barua ya wito wa Madeleka mbele ya kamati hiyo ya mawakili, ilisomeka, “tuhuma za kuvunja miiko ya kitaaluma kutoka kwa AG.”

Kwa mujibu wa barua za wito zilizosainiwa na Ngukah, Madeleka ametakiwa kufika mbele ya kamati Mei 13 na 14, 2024 kwa ajili ya kusikiliza kesi namba 02 ya 2024 itakayosikilizwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi Kivukoni Dar es Salaam.

Baada ya kesi hiyo, Madeleka pia anatakiwa kuhudhuria kesi namba 07 ya 2024 ambayo pia amefunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali itakayosikilizwa Mei 15 na 16 Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi.