Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Polisi asimulia alivyopigwa na waandamanaji

Muktasari:

  1. Askari Polisi wa kike aliyeonekana kwenye kipande cha video akipigwa na waandamanaji Jumatano ya Juni 25, 2025 nchini Kenya amesimulia namna alivyokumbana na kipigo hicho.

Kenya. Askari Polisi wa kike aliyeonekana kwenye kipande cha video akipigwa na waandamanaji Jumatano ya Juni 25, 2025 nchini Kenya amesimulia namna alivyokumbana na kipigo hicho.

Akisimulia kama alivyonukuliwa na Tuko News ya nchini humo, polisi huyo Konstebo Emily Kinya kwanza amewashukuru waandamanaji waliomuokoa kutoka kwenye kipigo kilichomsababishia majeraha mwilini.

Tukio hilo lilitokea Mtaa wa Muindi Mbingu jijini Nairobi, ndipo konstebo huyo aliangushwa kwa kupigwa na kitu kwenye mguu wake kisha waandamaji wakamvaa na kuanza kumshambulia.

Akiendelea kusimulia akiwa kitandani hospitali polisi huyo ambaye ni mama wa watoto wawili amesema waandamanaji waliwazidi nguvu maofisa hao ndipo walipoamua kurudi nyuma kabla ya kuanguka chini.

"Saa 1:30 usiku, mambo yalibadilika. Umati wa waandamanaji ukaanzisha vurugu na kuanza kutushambulia, hali ilipozidi kuzorota, maofisa walilazimika kurudi nyuma, lakini katika vurugu hizo, nilipigwa mguu.

“Nikajikwaa, nikaanguka waandamanaji waliojihami kwa mawe na silaha wakafika kwa hasira wakanipiga kichwani, nikapoteza simu na baadhi ya vifaa vya polisi,” amesema.

Lakini katikati ya vurugu hizo, kikundi kidogo cha waandamanaji kiliingilia kati na kumsaidia kisha kumpeleka mahali salama pia ndani ya gari la wagonjwa.

Konstebo Kinya, amesema amenusurika katika kile anachotaja kuwa mojawapo ya nyakati za kutisha zaidi maishani mwake. Katika simulizi hiyo amesema ‘Sisi pia ni binadamu’.

Maandamano hayo yalikuwa na dhumuni la kuadhimisha mwaka mmoja tangu vijana wa Gen-Z kuuawa kwenye maandamano yaliyofanyika mwaka 2024.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo, takriban watu 60 waliuawa mwaka jana na vikosi vya usalama katika wiki za maandamano ya kupinga ongezeko la ushuru na hali mbaya ya kiuchumi kwa vijana wa Kenya, pamoja na kupinga Mswada wa Sheria ya Fedha wa 2024.

Kufuatia hilo Gen-Z walipanga kufanya maandamano ya maadhimisho ambayo asubuhi yalikuwa ya amani ingawa muda ulivyozidi kwenda vurugu zikaibuka, ndipo hekaheka ilipoanza ikiwemo mabomu kurindima huku watu 16 wakiuawa.

Mamlaka nchini humo imetangaza kuwakamata watu 25 wanaoshukiwa kuharibu magari ya Serikali, mahakama na biashara.