Polisi yachunguza kifo kijana aliyefariki nyumbani kwa DJ
Kenya. Polisi wamesema watafukua mwili wa kijana Jeff Mwathi kisha kuendeleza uchunguzi kuhusu kifo chake. Mwathi alifariki katika mazingira ya kutatanisha baada ya mwili wake kukutwa katika nyumba ya msanii DJ Fatxo.
Kumekuwa na utata kuhusu kifo cha Jeff kilichotokea muda mfupi baada ya kutoka klabu na msanii DJ Fatxo.
Mkuu wa Polisi, Japheth Koome amesema wanatafuta ruhusa ya mahakama ili waweze kufukua mwili wa Jeff na kuufanyia uchunguzi wa kina kuhusu chanzo cha kifo chake.
Japheth Koome amesema kuna maswali ambayo yatajibiwa baada ya uchunguzi wa mwili wa kijana huyo.
"Lazima mwili huo ufukuliwe ili kuangalia uwezekano wa kutosha kupita katika dirisha analodaiwa aliruka," amesema Koome.
Polisi walisema wanajiandaa kwenda mahakamani ili waweze kupewa ruhusa ya kuutoa mwili wa Jeff.
"Tunakwenda mahakamani kuchukua kibali cha kufanya hivyo," amesema Koome.
Mwathi alikutana na Fatxo ili kupewa kazi ya kutengeneza mojawapo maduka yake. Kwenye video ambayo Mwathi alikuwa amemtumia mama yake kabla ya kukutana na Fatxo, kijana huyo alionekana kufurahia kuwa atakutana na msanii huyo.
Alimfahamisha mama yake kwamba wakikutana atapiga picha na kumtumia na kumwelezea jinsi makubaliano ya kikazi yatakavyokwenda.
Alifanya hivyo baada ya kukutana na msanii huyo lakini hakujua kuwa maisha yake yalikuwaukingoni.
Inaelezwa kuwa walikaa na Fatxo hata kuzunguka katika klabu kadhaa wakijivinjari na kisha saa tisa usiku siku iliyofuata wakaenda nyumbani kwa msanii huyo. Walikuwa pamoja na kina dada watatu na kufika nyumbani wakakutana na wanaume wengine wawili. Baadaye Fatxo aliondoka na kina dada hao na kumuacha Mwathi na wanaume hao wawili na ndipo kifo chake kikatokea.
Waliokuwa pamoja naye walidai kijana huyo aliruka kutoka ghorofa ya 10 hadi chini na ndipo alifariki papohapo.
Hata hivyo, kumekuwa na maswali na wapelelezi wa DCI wamesema kuna dalili kuwa aliuawa.
Imeandaliwa na Pelagia Daniel