Rais mteule Senegal azungumza, abainisha vipaumbele vyake

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Mamilioni ya wananchi wa Senegal walipiga kura Jumapili kumchagua rais wa tano wa nchi hiyo. Hatua hiyo imefuatia miaka mitatu ya msukosuko wa kisiasa ambao haujawahi kushuhudiwa ukizua maandamano makali dhidi ya Serikali na kuungwa mkono kwa upinzani.

Dakar. Mgombea wa upinzani Bassirou Diomaye Faye amesema watu wa Senegal wamechagua kuvunja mfumo wa sasa wa kisiasa huku akieleza vipaumbele vya Serikali yake atakayoiunda baada ya kutangazwa na kuapishwa.

Mpinzani mkuu wa Faye kutoka muungano unaotawala, Amadou Ba, tayari amekubali kushindwa katika kinyang'anyiro hicho na kusababisha tetemeko la kisiasa katika taifa hilo la Afrika Magharibi.

Ni ushindi wa kushangaza kwa Faye mwenye umri wa miaka 44, ambaye aliachiwa huru kutoka gerezani siku 10 tu kabla ya uchaguzi wa Jumapili Machi 24, 2024, hata hivyo matokeo yake bado hayajatangazwa rasmi.

Akizungumza katika hotuba yake ya kwanza kwa umma tangu Ba alipokubali kushindwa, Faye alieleza vipaumbele vyake muhimu ikiwemo kupambana na rushwa.

Moja ya vipaumbele vyake kuu kama Rais itakuwa “maridhiano ya kitaifa” kufuatia miaka mitatu ya machafuko na mzozo wa kisiasa, Faye amesema.

Faye pia ameapa kupambana na rushwa katika kila ngazi, kujenga upya taasisi na kukabiliana na gharama kubwa za maisha.

Ni mara ya kwanza katika chaguzi 12 za urais zilizofanyika nchini Senegal tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka kwa Ufaransa mwaka 1960, kwa mgombea wa upinzani kushinda katika duru ya kwanza ya upigaji kura.

Ba (62), alitambua ushindi wa Faye na kumpigia simu kumpongeza. Rais anayeondoka, Macky Sall ambaye hagombei tena baada ya kushinda mwaka 2012 na 2019, pia alimpongeza huku akisema ni “ushindi wa demokrasia ya Senegal”.

Kiu ya mabadiliko

Faye ameahidi ushirikiano na mrengo wa kushoto na kupitia upya mikataba ya gesi na mafuta, na Senegal kutokana na kuanza uzalishaji kwenye hifadhi ya mafuta na gesi iliyogunduliwa hivi karibuni baadaye mwaka huu.

Mgombea huyo wa upinzani hajawahi kushika nafasi ya kuchaguliwa kitaifa huko nyuma. Marekani ilimuunga mkono Sall katika kupongeza kwa ushindi wa demokrasia nchini Senegal.

“Kujitoa kwa watu wa Senegal katika mchakato wa demokrasia ni sehemu ya msingi wa urafiki wetu wa kina na uhusiano mkubwa wa nchi mbili,” msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Matthew Miller aliwaambia waandishi wa habari.

Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alimpongeza Faye kwa ushindi wake na kusema anatazamia kufanya kazi naye.

El Hadji Mamadou Mbaye, mhadhiri wa sayansi ya siasa na mtafiti katika Chuo Kikuu cha Saint-Louis, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba, “watu wana njaa ya mabadiliko unapoona kinachoendelea katika nchi hii katika masuala ya rushwa, kutoheshimu sheria”.

“Mtu ambaye aliwakilisha zaidi mabadiliko yaliyokuwa yakitamaniwa ni Ousmane Sonko”, Mbaye aliongeza, akimaanisha kinara wa upinzani ambaye alizuiwa kushiriki uchaguzi lakini akamwidhinisha Faye kama mbadala wake.

Faye alionekana wazi kuwa mbele ya Waziri Mkuu wa zamani, Ba, kulingana na matokeo ya awali kutoka kwenye vituo vya kupigia kura vilivyochapishwa na vyombo vya habari vya ndani na kwenye mitandao ya kijamii.

Matokeo rasmi yanatarajiwa kabla ya mwisho wa wiki. Idadi kamili ilihitajika kwa ushindi wa duru ya kwanza.

Awali, Senegal ilipaswa kufanya uchaguzi Februari 25, lakini kuahirishwa kwa saa 11 na Sall kuliibua mzozo mbaya zaidi wa kisiasa katika miongo kadhaa na ghasia zilizosababisha vifo vya watu wanne.

Takriban watu milioni 7.3 kati ya wakazi milioni 18 wa Senegal walijiandikisha kupiga kura.

Huku nchi hiyo ikionekana kuwa kinara wa demokrasia katika eneo la Afrika Magharibi linalokabiliwa na mapinduzi ambalo Russia inaimarisha ushawishi wake, uchaguzi huo ulifuatiliwa kwa karibu.

Ni mara ya tatu kwa Senegal kukabidhiana madaraka kidemokrasia kutoka kwa kiongozi mmoja aliyechaguliwa hadi mwingine tangu uhuru.

Mamia ya waangalizi kutoka mashirika ya kiraia, Umoja wa Afrika (AU), jumuiya ya kikanda ya Ecowas na Umoja wa Ulaya (EU) walikuwepo.

Baada ya wiki kadhaa za mkanganyiko, Baraza Kuu la Katiba la Senegal lilibatilisha jaribio la Sall la kuchelewesha uchaguzi hadi Desemba na kumlazimu kupanga upya tarehe hiyo hadi Machi 24, na kusababisha kampeni ya haraka ambayo iligongana na mfungo katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa Waislamu.

Urithi wa Sall katika utawala wake ni pamoja na kukamatwa kwa watu wengi, umasikini kuongezeka, asilimia 20 ya ukosefu wa ajira na maelfu ya wahamiaji wanaofanya safari za hatari kwenda Ulaya kila mwaka.

Matukio kadhaa ya machafuko yaliyochochewa kwa sehemu na mzozo kati ya Sonko na serikali yameshuhudia makumi ya watu wakiuawa na mamia kukamatwa tangu mwaka 2021.