Rais wa Senegal ampongeza mgombea wa upinzani kwa ushindi

Muktasari:

  • Faye ameonekana dhahiri kuwa mbele ya waziri mkuu wa zamani Ba mwenye umri wa miaka 62, kulingana na matokeo ya awali kutoka kwenye vituo vya kupigia kura vilivyochapishwa na vyombo vya habari vya ndani na kwenye mitandao ya kijamii.

Dakar. Rais wa Senegal anayemaliza muda wake, Macky Sall amempongeza mgombea wa upinzani, Bassirou Diomaye Faye kwa ushindi alioupata huku mshindani wake wa karibu, Amadou Ba akikubali kushindwa katika uchaguzi huo.

Baada ya mgombea huyo wa chama tawala, Amadou Ba kutambua ushindi wa Faye katika duru ya kwanza na kutoa pongezi zake, Sall, ambaye alishinda chaguzi za mwaka 2012 na 2019, amesema “napongeza maandalizi mazuri ya uchaguzi na nampongeza mshindi, Bassirou Diomaye Faye ambaye mwenendo wa kura unaonyesha kwamba ameshinda.”

Mgombea huyo wa upinzani aliyeshinda hajawahi kushika nafasi ya kuchaguliwa ya kitaifa na bado hajazungumza hadharani tangu uchaguzi wa Jumapili Machi 24, 2024, uliofuatia miaka mitatu ya machafuko na mgogoro wa kisiasa.

Mpinzani wake mkuu kutoka muungano wa chama tawala, Amadou Ba ametambua ushindi wa Faye katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo na akatoa pongezi zake, ilisema taarifa.

“Kwa kuzingatia mwelekeo wa matokeo ya uchaguzi wa urais na kusubiri kutangazwa rasmi, nampongeza Rais Bassirou Diomaye Diakhar Faye kwa ushindi wake katika duru ya kwanza,” Ba amesema katika taarifa hiyo.

Msemaji wa Serikali, Abdou Karim Fofana pia amesema kuwa Ba alimpigia simu mpinzani wake kumpongeza.

Faye ameonekana dhahiri kuwa mbele ya waziri mkuu wa zamani Ba mwenye umri wa miaka 62, kulingana na matokeo ya awali kutoka kwenye vituo vya kupigia kura vilivyochapishwa na vyombo vya habari vya ndani na kwenye mitandao ya kijamii.
Matokeo rasmi yanatarajiwa kabla ya mwisho wa wiki. Idadi kamili ilihitajika kwa ushindi wa duru ya kwanza.

Kurasa za mbele za magazeti zilikuwa tayari zimempongeza Faye. “Heri ya Siku ya Kuzaliwa Mheshimiwa Rais,” gazeti la Walf Quotidien limesema, likirejea leo Jumatatu kuwa siku ya kuzaliwa ya Faye.

Mamia ya wafuasi wa Faye waliokuwa na furaha walikuwa wamekusanyika katika makao makuu ya kampeni yake katika mji mkuu Dakar mwishoni mwa wiki.

“Ni mapinduzi kamili. Kila kitu kitabadilika. Kitabia, kijamii na kifedha, kila kitu kitabadilika,” Coumba Diallo, mwimbaji anayejulikana kama Queen Biz, alishangilia.
Takriban wagombea 10 kati ya 17 wamempongeza Faye mapema leo kutokana na matokeo ya awali yaliyochapishwa na vyombo vya habari.