Rais Novak wa Hungary ajiuzulu, Spika wa Bunge akaimu nafasi yake

Muktasari:
- Katalin Novak alifanya ziara ya kiserikali ya siku tatu nchini Tanzania Julai 17, 2023 na alifanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais Samia Suluhu Hassan. Pia, alitembelea maeneo mengine ikiwemo eneo la Fumvuhu lililopo wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Rais wa Hungary, Katalin Novak, mshirika wa karibu wa Waziri Mkuu, Viktor Orban, ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo kutokana na hasira ya umma juu ya msamaha uliotolewa kwa mtu aliyehusishwa na kesi ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto.
Muda mfupi baadaye mfuasi mwingine wa Orban, waziri wa zamani wa sheria, Judit Varga naye alitangaza kuwa anajiondoa kwenye utumishi wa umma kutokana na jambo hilo.
Uamuzi wa Novak kujiuzulu umetokana na shinikizo kubwa kutoka kwa wanasiasa wa upinzani na maandamano ya wananchi nje ya Ikulu ya Rais Ijumaa jioni.
“Ninajiuzulu wadhifa wangu,” alisema Novak (46), akikiri kwamba alifanya makosa.
“Ninaomba msamaha kwa wale niliowaumiza na waathiriwa wote wanaoweza kuwa na maoni kwamba sikuwaunga mkono,” alisema Waziri wa zamani wa Sera za Familia.
“Mimi niko, nilikuwa na nitabaki katika neema ya kulinda watoto na familia.”
Novak alikuwa mwanamke wa kwanza kushikilia nafasi ya urais katika taifa hilo Machi 2022.
Mzozo huo ulichochewa na msamaha aliopewa aliyekuwa naibu mkurugenzi wa makazi ya watoto. Alikuwa amesaidia kuficha tuhuma za unyanyasaji wa kingono za bosi wake kwa watoto waliowasimamia.
Uamuzi huo ulifanywa Aprili mwaka jana wakati wa ziara ya Papa Francis, mjini Budapest.
Tangu tovuti huru ya habari 444 ilipofichua uamuzi huo wiki iliyopita, upinzani nchini humo ulikuwa ukimtaka Novak ajiuzulu.
Ijumaa jioni Februari 9, 2024, waandamanaji walikusanyika nje ya Ikulu ya Rais na washauri watatu wa Rais walijiuzulu nyadhifa zao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na mgeni wake, Rais wa Jamhuri ya Hungary, Katalin Novak alipofanya zizara nchini Julai, 2023.
Novak, aliyekuwa Qatar kuhudhuria mechi ya Hungary dhidi ya Kazakhstan kwenye mashindano ya Dunia ya Maji ya Polo, alirejea Budapest haraka.
Mara tu ndege yake ilipotua aliibuka na kutangaza kujiuzulu.
“Msamaha uliotolewa na kukosekana kwa maelezo kunaweza kuzua mashaka juu ya kutovumilia kabisa kwa unyanyasaji kingono kwa watoto,” alisema.
“Lakini hakuna shaka juu ya suala hili,” aliongeza, kabla ya kuomba msamaha.
Dakika chache baada ya tangazo lake, mshirika mwingine wa Orban, Judit Varga, pia alitangaza “kujiondoa kwenye kwa maisha ya utumishi wa umma”.
Kama waziri wa sheria, wadhifa alioacha ili kuongoza zabuni ya uchaguzi katika Bunge la Ulaya, alikuwa ameidhinisha msamaha huo.
“Ninajiuzulu mamlaka yangu kama mbunge na mkuu wa orodha wa Bunge la Ulaya,” alisema kwenye ukurasa wake wa Facebook.
“Ilikuwa haraka: kwanza Novak, kisha Varga,” raia wa Hungary, Anna Donath, alinukuliwa na AFP.
“Lakini tunajua hakuna uamuzi muhimu unaweza kuchukuliwa nchini Hungary bila idhini ya Viktor Orban,” aliongeza Donath, mwanachama wa chama kidogo cha kiliberali cha Momentum, kwenye ukurasa wake wa Facebook.
“Lazima awajibike na kueleza kilichotokea... ni mfumo wake”.
Katika jaribio la kutuliza hasira ya taifa, Orban alikuwa ametangaza Alhamisi iliyopita kwamba alitaka kurekebisha katiba ya Hungary, ili kuondoa uwezekano wa kuwasamehe wahalifu wanaolawiti watoto.
Novak ambaye nafasi yake imechukuliwa kwa muda na Spika wa Bunge, Laszlo Kover, alitajwa mwaka jana na jarida la Forbes kama mwanamke mwenye ushawishi mkubwa katika maisha ya umma wa Hungary.
Kuondoka kwake kunaacha hali ya kisiasa ya Hungary kutawaliwa na wanaume. Tangu katikati mwa mwaka 2023 kumekuwa hakuna wanawake katika Baraza la Mawaziri lenye wanaume 16 wakiongozwa na Waziri Mkuu, Viktor Orban.