Rais Putin lawamani kwa kifo cha mwanaharakati wa upinzani Russia
Muktasari:
- Hali ya Navalny ilikuwa imezorota katika miaka yake mitatu gerezani ambapo alilalamika kunyimwa matibabu na alitumia takriban siku 300 katika kifungo cha upweke. Hadi wakati anakamatwa Januari 2021, alikuwa amekaa miezi kadhaa tangu alipopona ugonjwa wa shambulio la neva.
Moscow. Wakati kifo cha mwanaharakati wa upinzani nchini Russia, Alexei Navalny kikiwa cha utata, familia ya mwanasiasa huyo imemnyooshea kidole Rais wa nchi hiyo, Vladmir Putin kuhusika katika kifo hicho cha mpendwa wao.
Jumamosi iliyopita, familia ya Navalny ilithibitisha kwamba mwanaharakati huyo wa kisiasa alifariki saa 8:17 mchana, Februari 16, mwaka huu.
Mamlaka katika gereza alilokuwa amefungwa ilisema alifariki ghafla. Hata hivyo, haijulikani mwili wake upo wapi na kama umefanyiwa uchunguzi kubaini chanzo cha kifo chake.
Mama yake Navalny, Lyudmila Navalnaya ambaye alifika eneo hilo Jumamosi iliyopita, alitembelea chumba cha kuhifadhia maiti katika mji wa Salekhard karibu na gereza hilo, ambapo aliambiwa mwili wake umepelekwa.
Msemaji wa mwanasiasa huyo, Kira Yarmysh amesema Lyudmila hakuruhusiwa kuingia ndani ya kituo hicho na kwamba wakili wa mwanawe walitolewa nje ya jengo hilo. Wafanyakazi hawakuthibitisha kama mwili wake ulikuwepo hospitalini hapo.
Kwa mujibu wa Yarmysh, uchunguzi wa kamati ya Russia kuhusu kifo hicho umesogezwa mbele kwa muda usiojulikana.
Tayari alikuwa ameambiwa na maofisa kwamba mwili wa Navalny hautakabidhiwa kwa familia yake hadi uchunguzi huo ukamilike.
Yarmysh baadaye amesema wachunguzi walimwambia Lyudmila kwamba hawatakabidhi mwili kwa wiki mbili kwa kuwa watakuwa wakifanya ‘uchambuzi wa kemikali’.
Hali ya Navalny ilikuwa imezorota katika miaka yake mitatu gerezani ambapo alilalamika kunyimwa matibabu na alitumia takriban siku 300 katika kifungo cha upweke. Hadi wakati anakamatwa Januari 2021, alikuwa amekaa miezi kadhaa tangu alipopona ugonjwa wa shambulio la neva.
Hata hivyo, alionekana kuwa na afya tele katika video ya mahakamani siku moja kabla ya kifo chake.
Kifo cha kiongozi huyo wa upinzani ni mwendelezo wa mauaji ya wapinzani wa Rais Putin na serikali yake, na amekuwa akihusishwa navyo moja kwa moja katika utawala wake.
Boris Nemtsov, kiongozi wa upinzani mwenye mvuto ambaye alikuwa Naibu Waziri Mkuu miaka ya 1990, alipigwa risasi nne mgongoni mbele ya Ikulu ya Russia (Kremlin) mwaka 2015.
Anna Politkovskaya, mwandishi wa habari ambaye aliandika vitabu kuhusu dola ya kipolisi ya Russia chini ya Vladimir Putin, aliuawa mwaka 2006 na wauaji waliokodiwa ambao walilipwa kwa mujibu wa hakimu katika kesi yao, na mtu asiyejulikana.
Mmoja wa wauaji wake baadaye alipigana nchini Ukraine na sasa amesamehewa.
Alexander Litvinenko, wakala wa zamani wa kikosi cha kijasusi cha KGB na mkosoaji wa Putin, alifariki mjini London mwaka 2006, wiki tatu baada ya kunywa kikombe cha chai kilichokuwa na kiambata hatari cha mionzi.
Uchunguzi wa Uingereza uligundua kuwa Litvinenko alitiwa sumu na mawakala wa FSB Andrei Lugovoi na Dmitry Kovtun, ambao walikuwa wakitenda kwa amri ambazo pengine ziliidhinishwa na Putin.
Hata hivyo, Ikulu ya Kremlin haitoi maelezo yoyote kuhusu vifo hivi wala kukanusha kuhusika navyo.
Jake Sullivan, mshauri wa usalama wa taifa nchini Marekani, Ijumaa alielezea kifo cha Navalny kama msiba mbaya na mfano wa hivi karibuni wa historia ndefu na chafu ya serikali ya Russia ya kuwadhuru wapinzani wake.
Wakati huohuo, Mahakama katika eneo la Kaskazini mwa Russia, mwezi ujao itasikiliza kesi iliyofunguliwa na mama yake kiongozi huyo wa upinzani, washirika wake walisema Jumatano.
Lyudmila Navalnaya amesafiri hadi gereza la mbali la IK-3 ambalo mwanaye amefia, lakini tangu Jumamosi iliyopita, alipofika, amezuiwa kuuona mwili wake.
Jumanne iliyopita, alitoa wito kwa Rais wa Russia, Vladimir Putin kuachiliwa kwa mwili wa mtoto wake.
Shirika la habari la TASS liliripoti kuwa mahakama ilipokea malalamiko juu ya ‘vitendo haramu’ na kwamba kusikilizwa kwa kesi hiyo kutafanyika kwa uwazi.
Timu ya Navalny imesema kwenye mitandao ya kijamii kwamba mahakama katika mji wa Arctic wa Salekhard itasikiliza kesi hiyo Machi 4, mwaka huu, zaidi ya wiki mbili baada ya mpinzani huyo wa Putin kufariki.
“Nakuomba, Vladimir Putin. Suluhu la suala hilo linakutegemea wewe tu,” amesema.
“Niruhusu nimuone mwanangu, nataka mwili wa Alexei utolewe mara moja ili nimzike kwa njia ya kibinadamu.”
Mjane wa Navalny, Yulia Navalnaya ameunga mkono wito huo, akitaka mamlaka kuruhusu azikwe kwa heshima.
Hata hivyo, Putin hajatoa maoni wala kujibu. Kiongozi huyo wa muda mrefu wa Russia amekuwa kimya juu ya kifo cha mpinzani wake mkuu wa kisiasa.