Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Ruto akubali yaishe, sasa kuzungumza na waandamanaji

Muktasari:

  • Baada ya maandamano ya kupinga muswada wa sheria ya fedha ya mwaka 2024/25 kutikisha nchini Kenya, Rais wa nchi hiyo amesema yuko tayari kuzungumza na waandamanaji.

Kenya. Taarifa zinaeleza kuwa Rais wa Kenya, William Ruto atafanya mazungumza ya wazi na vijana kuhusu kukerwa na hali ya mambo nchini humo.

Kiongozi huyo amesema hayo wakati maelfu ya vijana wakiandamana kona mbalimbali kupinga muswada wa sheria ya fedha ya mwaka 2024/25 wakidai ni mwiba kwa Wakenya.

Leo Jumapili Juni 23 2024, Rais Ruto na  naibu wake, Rigathi Gachagua wameshiriki ibada katika Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya ACK, Nyahururu, Kaunti ya Laikipia wakiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.

Rais Ruto amesema yuko tayari kwa mazungumzo na maelfu ya waandamanaji hao ambao ni vijana wanaopinga mapendekezo ya nyongeza ya ushuru katika bidhaa mbalimbali huku akisisitiza kukutana ili kujenga Taifa hilo kwa pamoja.

Katika hilo, msemaji wake Hussein Mohamed kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) amesema:"vijana wetu wamejitokeza kujihusisha na masuala ya nchi yao. wametimiza wajibu wao wa kidemokrasia, kusimama na kutambuliwa. Ninajivunia wao."

"Tutakuwa na mazungumzo nanyi ili kutambua masuala yenu na kufanya kazi pamoja kama taifa," amesem Mohamed a.

Pia, Tovuti ya Citizen Digital ya nchini humo imesema katika ibada hiyo, Askofu Mkuu wa Kianglikana, Jackson Ole Sapit amemtaka Rais Ruto kuwaamuru maofisa wa polisi kuacha kutumia nguvu wakati wa maandamano kwa vile wamekuwa wakiandamana kwa amani barabarani.

"Huu ni wakati wa kupambanua. Tukumbatie roho ya kusikiliza zaidi kuliko kuzungumza. Hata katika haya yanayoendelea, hao ni watoto wa familia zetu tusitumie nguvu nyingi lakini pia tunawasihi wasiwe wavunja sheria na kuharibu, kuwalemaza au kuua,” amesema Sapit.

Maandamano yameandaliwa kwenye mitandao ya kijamii na kuongozwa kwa kiasi kikubwa na Wakenya wanaojiita Gen-Z yameshika kasi yakidai kutoridhika na sera za kiuchumi za Ruto ambapo yamesababisha vifo vya raia wawili na majeruhi.

Hata hivyo, Jumanne ya Juni 25, Gen-Z wamepanga kuandamana zaidi japokuwa hakuna majibu waliyoyatoa hadi sasa kufuatia tamko hilo la Rais Ruto. Wamepanga maandamano ya siku saba yanatarajiwa kuanza kuanzia Jumatatu, Juni 24 ili kuongeza shinikizo zaidi kwa serikali kuutupilia mbali muswada huo kwa ujumla

Hadi sasa, watu wawili wamefariki na makumi kujeruhiwa katika maandamano yaliyofanyika Alhamisi katika mji mkuu Nairobi karibu na Bunge yakiwa na purukushani za kurushwa kwa mabomu ya machozi, hii ni kulingana na wanaharakati wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa ofisa wa Tume ya Haki za Kibinadamu ya Kenya, Evans Kiratu mwenye umri wa miaka 21 alipigwa na bomu la machozi wakati wa maandamano na kufariki dunia akiwa hospitalini.

Pia, Ijumaa, Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) ilisema inachunguza madai kwamba mwanaume mwenye umri wa miaka 29 alipigwa risasi na maofisa jijini Nairobi baada ya maandamano hayo.

Mashirika kadhaa, ikiwa ni pamoja na Amnesty International Kenya, yamesema takriban watu 200 walijeruhiwa jijini Nairobi katika maandamano ambayo yalishuhudia maelfu ya watu wakiingia mitaani kote nchini.