Ruto na urais wake, Gachagua Mlima Kenya, taifa njiapanda

Watu wawili, mmoja mwenye maarifa makubwa ya biashara, mwingine alibeba mtaji mkubwa, waliungana kusaka mafanikio waliyonayo hivi sasa. Wakiwa kileleni, kila mmoja anajiona ndiye nguzo kuu ya mafanikio.

Mwenye mtaji anajinasibu kuwa kwa maarifa yake, angeweza kuungana na yeyote mwenye mtaji na kufikia mafanikio waliyonayo. Aliyebeba mtaji, yeye anaona bila yeye hakuna ambacho kingewezekana. Kadiri kila mtu anavyovutia kamba kwake, ndivyo uhusiano wa wawili unavyojenga afya mgogoro.

Hiyo ndiyo tafsiri ya mgogoro wa Rais wa Kenya, William Ruto na Naibu Rais, Rigathi Gachagua. Ndani ya kila mmoja kuna ufahari na majivuno ya kile ambacho alikichangia kwenye Uchaguzi Mkuu Kenya mwaka 2022, hadi kuvuna nafasi walizonazo sasa.
 

Kiini cha mgogoro

Katika kamusi ya kisiasa kuna msemo wa wakati wa uchaguzi unaoitwa "kangaroo ticket". Tafsiri yake ni pale chama au kambi fulani inapoingia kwenye uchaguzi, hasa wa urais, halafu mgombea mwenza anakuwa turufu kuliko mgombea urais.

Yaani, wakati wa uchaguzi, watu wanashawishika kumchagua mgombea A awe rais kwa sababu ya mgombea mwenza wake. Hiyo ndiyo inaitwa

"kangaroo ticket". Kuelekea Uchaguzi Mkuu Kenya mwaka 2022, wagombea urais waliokuwa na nafasi kubwa ni Ruto na Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Raila Odinga.

Tabia ya upigaji kura Kenya na mgawanyo wa idadi ya wapigakura Kenya, kwa pamoja viliwalazimisha Raila na Ruto kucheza karata ya kangaroo ticket kwenye eneo la Mlima Kenya. Kila mmoja hakuwa na namna zaidi ya kuteua mgombea mwenza kutoka eneo hilo.

Raila anatokea Nyanza, Ruto ni wa Rift Valley. Hali ilivyokuwa, Mlima Kenya haikuwa na mgombea urais mwenye nguvu. Kimantiki, yeyote, kati ya Raila na Ruto, angechanga karata zake vema Mlima Kenya, angeweza kujipatia uungwaji mkono mzuri.

Raila alikuwa akiungwa mkono na Rais wa Nne wa Kenya, Uhuru Kenyatta, ambaye asili yake ni Mlima Kenya. Vilevile, tangu mwaka 2013, Mlima Kenya ilikuwa ngome ya Uhuru na alijizolea mamilioni ya kura kwenye uchaguzi wa mwaka 2013 na 2017.

Kuelekea Uchaguzi Mkuu Kenya 2022, kiasi ambacho Raila aliungwa mkono Mlima Kenya ni kikubwa kulinganishwa na wakati wowote alipogombea urais. Ni kwa sababu ya kuungwa mkono na Uhuru pamoja na chama chake, Jubilee.

Kwa mujibu wa rekodi za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Kenya, Mlima Kenya walikuwa na wapigakura milioni 5.9 kuelekea Uchaguzi Mkuu 2022. Kwa mgawanyo, Mlima Kenya Magharibi walikuwa na kura milioni 4.6 na Mlima Kenya Mashariki milioni 1.3.

Eneo la Nyanza, anakotokea Raila walikuwa na wapigakura milioni 2.9, Rift Valley kwa Ruto ni milioni 2.4, sawa na Nairobi. Eneo la Magharibi ya Kenya na Pwani kulikuwa na wapigakura milioni 3.9, kwa mgawanyo wa milioni 2.1 Magharibi na 1.8 Pwani.

Ukambani palipo na ngome ya Kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, kulikuwa na wapigakura milioni 1.6. Maeneo mengine namba za wapigakura ni chini ya milioni moja. Ni kwa sababu hiyo, Mlima Kenya lilikuwa eneo lenye kutolewa macho na kila mgombea urais.

Kisha, Ruto alimteua Gachagua kuwa mgombea mwenza wake, Raila akamchukua Martha Karua. Wote wawili, Gachagua na Karua ni watu wa Mlima Kenya, ambalo ni eneo la jamii ya Wakikuyu. Tabia ya upigaji kura Kenya hutazama ukabila na maeneo. Ni kwa kutambua hilo, Raila na Ruto, walikosa chaguo zaidi la mgombea mwenza zaidi ya kuangukia Mlima Kenya.
 

Haijafikia miaka miwili

Septemba 13, 2022, Ruto alikula kiapo kuwa rais, siku hiyohiyo, Gachagua alitawazwa unaibu rais. Ni pungufu ya miaka miwili tangu tukio hilo. Gachagua hazungumzi tena yale maneno aliyoyatamka siku alipoteuliwa na Ruto kuwa mgombea mwenza. Gachagua wa sasa anakumbatia nguvu zake Mlima Kenya.

Kama hadithi ya maskini na wanaye, tajiri na mali zake. Gachagua anarejea Mlima Kenya na kukumbatia watu. Anamwalika mpaka Uhuru, ambaye alikuwa hasimu wao kwenye uchaguzi uliopita, ili wajenge ushirikiano wa pamoja kwa watu wa Mlima.

Miaka miwili iliyopita, Gachagua alipoteuliwa kuwa mgombea mwenza, alisema yeye ni mtiifu kwa Ruto, tofauti na viongozi wengine ambao alidai baadaye wangekuja kumsumbua, kipindi ambacho angekuwa ameshakalia kiti cha urais wa Jamhuri ya Kenya.

"Watu walisema Ruto akiniweka mimi kuwa naibu wake nitasababisha usumbufu, lakini hilo siyo la kweli. Kama umekulia kwenye familia yenye umoja kama mimi, huwezi kubadilika unapokuwa mkubwa. Mimi ni mtu ambaye nimekuwa nikinyooka maisha yangu yote. Lugha ninayojua ni 'ndiyo mkuu' kwa bosi wangu," alisema Gachagua.

Uhusika wa sasa wa Gachagua, haufanani na maneno aliyoyasema miaka miwili iliyopita. Aliahidi utiifu usiyoyumba kwa Ruto, lakini sasa hivi anamtetemesha kwa mtaji wake. Gachagua anajipambanua kuwa samaki mkubwa (the kingpin) wa Mlima Kenya, kwake ni fahari kutambulika ni jogoo wa Mlima kuliko unaibu rais. Anatishia kwamba haoni shida kuacha unaibu rais.

Ruto wa miaka miwili iliyopita, alipomteua Gachagua alisema: "Nawahakikishia kuwa Rigathi ni mtu makini na nilikuwa natafuta mtu makini. Nina imani sana na yeye kwa sababu Wakenya wanahitaji watu makini kama yeye ili kuzikabili changamoto za taifa letu. Nimechagua Rigathi kwa sababu anajali maisha ya watu, ni mchapakazi ambaye huwa anakabili changamoto bila woga."

Uhusika wa Ruto wa sasa, Gachagua anatoa maagizo kwa umma, naye anatoa hotuba kupinga, halafu anaunga mkono kile kilichokemewa na naibu wake. Mfano mmojawapo ni hivi karibuni, Gachagua aliwataka wabunge kufanya kazi kwenye maneo yao na kuacha kutembea sehemu ambazo zina wawakilishi wengine. Ruto alitetea hadharani wabunge kuzunguka popote ili kufanya kazi ya usimamizi wa serikali.


Nani kawafikisha hapo?

Haijawahi kuwa salama kwa watu wawili kujiona wana mchango sawa kwenye mamlaka. Mwanzoni Gachagua alikuwa mnyenyekevu kwa sababu alifahamu fika kuwa bila Ruto, asingekuwa naibu rais. Hivi sasa, Gachagua anatambua kwamba yeye alikuwa tiketi ya kangaroo, iliyomfanya Ruto kukubalika Mlima Kenya, hivyo kushinda urais.

Gachagua anatamani Ruto autambue mchango wake, ndiyo maana anaamua kucheza sanaa ya kuwaunganisha Mlima Kenya, huku akipambanua kuwa samaki mkubwa wa eneo hilo. Kisha, Gachagua anatoa tamko kuwa haitatokea tena kingpin wa Mlima Kenya akatupiwa mawe, kama alivyofanyiwa Uhuru Uchaguzi Mkuu Kenya 2022.

Sanaa hiyo ya Gachagua, bila shaka ni kumtisha Ruto, atambue kuwa asipomnyenyekea na wakasafiri vizuri, anaweza kumfanya akose uungwaji mkono Mlima Kenya katika Uchaguzi Mkuu Kenya 2027. Tafsiri ya anachokifanya Gachagua ni kama anamwambia Ruto: "Wewe na urais wako, mimi na mtaji wangu wa Mlima Kenya."

Wakati huohuo, wanaomuunga mkono Ruto, wanamwambia Gachagua achague unaibu rais au aachie ngazi, halafu Uchaguzi Mkuu Kenya 2027, agombee ugavana kwenye kaunti ya Nyeri, ambayo ndiyo ngome kuu ya Gachagua. Mbunge wa Kimilili, Didmus Barasa, alimtaka Gachagua kumheshimu Ruto, kwani nafasi hiyo alipewa kwa heshima, lakini hakustahili.

Hata Ruto mwenyewe katika siku za karibu, amenukuliwa akisema ni yeye aliyemteua Gachagua, licha ya kukataliwa ndani ya muungano wao wa Kenya Kwanza. Bila shaka, alitaka jamii imwone Gachagua kama mtu asiyetosheka na asiye na shukurani.