Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rais Ruto atetea kauli yake kuhusu kutotii amri ya Mahakama

 Rais wa Kenya Dk William Ruto

Muktasari:

  •  Rais Ruto amesisitiza kuwa Mahakama isiyo na uadilifu, ni jambo ambalo halikubaliki Kenya

Kenya. Rais wa Kenya Dk William Ruto amelazimika kutoa ufafanuzi huku akitetea kauli yake ya kutotii amri za Mahakama zilizotolewa na majaji baada ya wadau nchini humo kumkosoa kwa kauli hiyo.

Ruto amesisitiza kuwa Mahakama isiyo na uadilifu, ni jambo ambalo halikubaliki Kenya.

Mtandao wa Nation umeripoti kuwa, jana Jumatano Januari 3, 2024; Jaji Mkuu Martha Koome na Kiongozi wa Upinzani, Raila Odinga walisema kwa kukiuka utawala wa sheria, kiongozi wa nchi atakuwa anaweka msingi wa machafuko.

Hata hivyo, kupitia taarifa ya Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto amesema rushwa ndani ya Mahakama, serikalini, bungeni au miongoni mwa wananchi, haitakiwi kukingwa na uhuru wa Mahakama.

"Ni jukumu letu kufichua na kuwawajibisha wale wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi, haijarishi ni kina nani na wapo wapi. Itakuwa ni kosa la kukiuka kiapo cha Rais na kusaliti matakwa ya watu kuwaruhusu matumaini yao na ndoto zao kuzuiliwa na rushwa na ukwasi," amesema Rais Ruto.

Katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Msemaji wa Ikulu hiyo, Hussein Mohamed, Rais pia ametoa shutuma dhidi ya Chama cha Wanasheria Kenya (LSK), akisema hakina mamlaka ya kumshauri kuhusu masuala ya katiba na uhuru wa Mahakama.

Ruto amesema ushawishi wa masilahi binafsi na maofisa wa Mahakama wenye kujihusisha na vitendo vya rushwa, lazima ukome.

"Historia inaonyesha Kenya imekwamishwa na watu wachache wala rushwa na wale wenye masilahi binafsi wanaokwamisha maendeleo jumuishi ya Taifa. Huu ni wakati wa kuandika historia mpya ya nchi yetu, tutavunja minyororo ufisadi,” amesema Rais Ruto.

Pia, amesema kama muumini wa Katiba, anatambua umuhimu wa kuongoza kwa mfano katika kuilinda katiba, ikiwa ni pamoja na kulinda raia wa Kenya kutokana na kutokuwepo kwa uadilifu katika mhimili wa Mahakama, uliofanywa na maofisa wala rushwa.

Majibu ya Rais yalikuja saa kadhaa baada ya kiongozi wa Azimio la Umoja, Raila Odinga, kumtaka Dk Ruto kuheshimu mihimili mingine, huku akimsihi kutoingilia uhuru wa Mahakama.

Odinga amemshutumu Rais Ruto kwa kujaribu kuwatisha majaji na mahakimu ili wasisikilize kesi dhidi ya sera zake, kuondoa kesi hizo au kutoa uamuzi kwa upande wake.

"Ilikuwa matumaini yangu kwamba baada ya machafuko na maumivu yaliyopatikana mwaka 2023, ambayo Wakenya bado wanateseka kutokana nayo, utawala wa Kenya Kwanza ungeanza mwaka huu mpya na mawazo na unyenyekevu zaidi huku wakijifunza kutokana na yaliyopita," Odinga amesema.

"Tuna mpango mwaka huu wa kulazimisha Serikali ya sasa kushughulikia masuala kadhaa yanayoathiri Wakenya," amesema Odinga.

Pia, amemwambia Rais Ruto atambue kwamba, bima yake bora ni kuitii sheria na hakuna njia nyingine.

Hata hivyo, Jaji Mkuu Martha Koome ameonya kauli ya Rais Ruto dhidi ya vitisho vya kutotii amri za Mahakama, akisema hatua hiyo inaleta hatari ya machafuko nchini.

Katika taarifa yake kwa majaji na maofisa wa mahakama iliyochapishwa na Gazeti la Nation, Jaji Mkuu ameonya kwamba wakati maofisa wa umma au wa Serikali wanatishia kutotii amri za Mahakama, hivyo utawala wa sheria unapungua thamani.

Bila kutaja jina la Rais Ruto, Jaji Mkuu amesema kukaidi amri za Mahakama ni ukiukaji wa uaminifu kwa umma uliowekwa kwa maofisa wa umma na Serikali ambao wanapaswa kila wakati kutenda sawa sawa na matakwa ya sheria na katiba.