Rais Xi Jinping kukutana na Rais Putin Moscow

Rais wa China Xi Jinping.

Muktasari:

  • Rais wa China Xi Jinping anatarajia kuwasili nchini Russia Machi 20, kuzungumza na Rais wa nchi hiyo Vladimir Putin kuhusu ushirikiano wa kimkakati.

Moscow. Taarifa kutoka Ikulu ya Kremlin nchini Russia, imeeleza kuwa Rais wa China Xi Jinping atasafiri hadi Moscow wiki ijayo kufanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo, Vladimir Putin, kuhusu ushirikiano wa kimkakati.

Kwa mujibu mtandao wa BBC, ziara hiyo inajiri baada ya Beijing, mshirika wa Russia kutoa mapendekezo ya kumaliza vita nchini Ukraine.

Licha ya China kutoa mapendekezo hayo, nchi za Magharibi zimeionya China dhidi ya kuipatia Russia silaha.

Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilisema Xi atakuwa nchini Russia kuanzia Machi 20 hadi 22 kwa mwaliko wa Putin.

Msemaji wa wizara hiyo, Hua Chunying, amesema “China itashikilia msimamo wenye lengo na haki kuhusu vita vya Ukraine na kuchukua jukumu la kujenga katika kuendeleza mazungumzo ya amani.”

Februari Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky alisema alitaka kukutana na Xi ili kuamini kwamba China haitasambaza silaha kwa Russia.

Baadhi ya vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti kuwa Xi na Zelensky watazungumza kwa simu baada ya ziara ya kiongozi huyo wa China mjini Moscow, lakini hilo bado halijathibitishwa.

Ukraine inaamini kuwa Rais Xi anafanya ziara hiyo ili kutuma ishara kwa ulimwengu kwamba Russia nayo ina washirika.