Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Russia yashambulia Kyiv kwa mamia ya droni na makombora, watu 30 wauawa

Kyiv. Russia imefanya mashambulizi kwa mamia ya ndege zisizo na rubani (droni) na makombora dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, alfajiri ya Alhamisi na kusababisha vifo vya watu takribani 30, kujeruhi wengine 91 na kuharibu takriban majengo 130 katika shambulizi baya zaidi kuwahi kulikumba jiji hilo mwaka huu.

Milipuko ilisikika katika maeneo mbalimbali ya Kyiv usiku huku maelfu ya wakazi wakikimbilia kwenye maeneo ya kujikinga na mashambulizi pamoja na vituo vya treni ya chini ya ardhi.

Vikosi vya kutoa huduma za dharura na uokozi vya Ukraine vilisema idadi ya vifo iliongezeka baada ya miili zaidi kupatikana kwenye vifusi, huku vikosi vya uokoaji vikiendelea kutafuta manusura.

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, aliyekatisha ziara yake nchini Ireland na kurejea Kyiv, alitembelea moja ya majengo ya makazi yaliyoharibiwa vibaya na kusema kuchelewa kwa washirika wa Ukraine kutekeleza ahadi zao za kuipatia nchi hiyo mifumo ya ulinzi wa anga, kumechangia ukubwa wa uharibifu huo.

"Kama washirika wetu wangetekeleza ahadi zao kwa wakati, naamini tungeweza kuokoa nyumba na maisha zaidi. Tunachowaomba ni kutekeleza tulichokubaliana, si zaidi ya hapo," alisema.

Aidha, alisema kuimarishwa kwa ulinzi wa anga kutakuwa miongoni mwa masuala muhimu katika mkutano ujao wa Nato, akisisitiza kuwa Ulaya inapaswa kuwa na uwezo wa kujilinda dhidi ya mashambulizi ya makombora ya balestiki.

Jeshi la Anga la Ukraine lilisema Urusi ilirusha makombora 74 na droni 496 katika mashambulizi ya usiku mmoja, huku likieleza kuwa idadi kubwa ya makombora ya balestiki na upungufu wa makombora ya mfumo wa Patriot ulifanya iwe vigumu kuyazuia mashambulizi hayo.

Kwa upande wake, Wizara ya Ulinzi ya Russia ilisema mashambulizi hayo yalikuwa ya kulipiza kisasi na yalilenga viwanda vya kijeshi pamoja na miundombinu inayohusiana na sekta ya ulinzi katika mji wa Kyiv na Mkoa wa Kyiv.

Moscow ilidai operesheni hiyo ililenga maeneo yanayotengeneza mifumo ya makombora na vituo vya kusambaza nishati vinavyosaidia shughuli za viwanda hivyo.

Kwa mujibu wa Russia, maeneo yaliyoshambuliwa yanajumuisha Kiwanda cha Redio cha Kyiv, Kampuni ya Radiyoniks na maghala yanayodaiwa kuhifadhi ndege zisizo na rubani pamoja na vipuri vyake, ikidai mashambulizi hayo yamevuruga uzalishaji wa mifumo ya makombora inayotumiwa na Jeshi la Ukraine.

Russia ilisema mashambulizi hayo yalifanyika kujibu kile ilichokiita mashambulizi ya Ukraine dhidi ya miundombinu ya kiraia ndani ya eneo lake, ikidai baadhi ya makombora yaliyokuwa yakitengenezwa katika viwanda hivyo yalikuwa yakitumika kushambulia malengo ndani ya nchi hiyo.

Kuhusu uharibifu wa majengo ya makazi mjini Kyiv, Moscow ilikanusha kuyashambulia moja kwa moja na kudai sehemu ya uharibifu huo ulisababishwa na makombora ya ulinzi wa anga ya Ukraine yaliyoshindwa kufikia malengo yake na kulipuka angani.

Hata hivyo, Ukraine na washirika wake wa Magharibi wameendelea kusisitiza kuwa mashambulizi ya Urusi yamelenga na kuathiri maeneo ya kiraia, huku pande zote zikiendelea kutoa maelezo yanayokinzana kuhusu kilichotokea.


Imeandikwa na msaada wa REUTERS