Sura mbili ziara ya Rais Ruto Marekani

Rais wa Kenya, Rais William Ruto na Rais wa Marekani, Joe Biden na wakeze zao, Rachel Ruto, Jill Biden wakipunga mkono katika Ikulu ya Marekani.
Muktasari:
Rais Biden amesema nchi hizo mbili zina wasiwasi sawa wa usalama kutoka kwa makundi ya kigaidi kama ISIS na msaada kwa Ukraine dhidi ya uvamizi wa Russia.
Dar es Salaam. Wakati Rais wa Kenya, William Ruto akiendelea na ziara yake nchini Marekani, kumekuwa na maoni kuhusu manufaa ya ziara hiyo, huku faida na hatari zake zikitajwa.
Katika ziara hiyo ya siku nne, Rais Ruto anatarajiwa kukutana na viongozi wa mabunge yote mawili ya Marekani ambapo atawaomba waunge mkono ajenda ya mageuzi ya bara Afrika kwenye mfumo wa utoaji mikopo kutoka kwa taasisi za kimataifa za fedha.
Akizungumza na Ruto katika Ikulu ya Marekani, Rais Joe Biden ametangaza kuwa atashauriana na Bunge ili kuifanya Kenya kuwa mshirika mkuu asiyekuwa mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya Mataifa ya Magharibi, (NATO) kuimarisha ushirikiano wa kiusalama.
Rais Biden amesema nchi hizo mbili zina wasiwasi sawa wa usalama kutoka kwa makundi ya kigaidi kama ISIS na msaada kwa Ukraine dhidi ya uvamizi wa Russia.
Kwa upande wake Rais Ruto alisema ushirikiano huo utainua mchango wa nchi yake katika uimarishaji wa amani katika Pembe ya Afrika.
Pia amesisitiza kujitolea kwa serikali yake kuongoza ujumbe wa kimataifa wa usaidizi wa usalama nchini Haiti.
Kenya itakuwa taifa la kwanza la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kuteuliwa kuwa mshirika mkuu asiyekuwa mwanachama wa Nato.
Nchi nyingine zilizoteuliwa ni pamoja na Morocco, Misri na Tunisia.
Hadhi ya mshirika mkuu asiyekuwa mwanachama wa Nato, huwapa washirika wa kigeni fursa ya upendeleo wa kijeshi na kiuchumi kutoka Marekani.
Ruto atakuwa kiongozi wa kwanza wa Afrika katika zaidi ya miaka 15 kufanya ziara rasmi ya kiserikali nchini Marekani.
Hii ni fursa kwa Rais Joe Biden kudhihirisha kujitolea kwa Afrika wakati ambapo Washington inaonekana kuwa na ushawishi katika ushirikiano wake na bara hilo.
Lakini uhusiano na washirika wengine wa Kiafrika unakabiliwa na mvutano, kwani wapinzani wa kimkakati ikiwa ni pamoja na Russia na China zinaonyesha upinzani katika maeneo ya jadi ambayo yamekuwa na ushawishi wa Magharibi.
Sura mbili
Akiichambua ziara hiyo, mhadhiri katika chuo cha Diplomasia Dar es Salaam, Deus Kibamba alisema:
“Ni funzo zuri kwamba Kenya imekuwa ikijitahidi kujenga hoja kwamba Kenya inafaa katika uhusiano wa kimataifa. Kwa sababu hii sio ya kwanza kwa Kenya, Rais Uhuru Kenyatta alifanya mara mbili kwa Marekani peke yake, kwa hiyo huu ni mwendelezo,” amesema.
Katika suara ya pili, Kibamba amesema ni funzo gumu na ndio sababu ya kuifanya ziara iwe ya kitaifa.
“Kenya inahitajiwa sana na Marekani. Yupo rais mmoja wa Marekani aliwahi kusema nchi hiyo haina rafiki wala adui wa kudumu, bali ina masilahi ya kudumu,” amesema.
Akifafanua zaidi, Kibamba anasema Marekani inaihitaji sana Kenya kama eneo la kuweka vituo vyake vya kijeshi katika kuingia kwenye ukanda wake wa Afrika.
“Ndio maana imeitambulisha Kenya kwa Nato kama mdau muhimu. Kwamba inaweza kuitumia ardhi yake, inaweza kuyapa mafunzo majeshi yake na kuyatumia kwenye sehemu za hatari.
“Maana Marekani huwa haitumii majeshi yake kwenye sehemu hatari, bali inapeleka majeshi mengine.
“Tunaweza kujikuta Kenya inapiganishwa vita ambayo si yake, ndio maana unaona wanatakiwa wapeleke polisi wao nchini Haiti.
“Mwalimu Nyerere alikuwa anaita mercenaries (wanajeshi wa kukodiwa), angesema hapa ni heri tubaki na umasikini wetu,” amesema.
Amefaanua kuwa Marekani inashindana na Russia na China katika kuidhibiti Afrika.
“Ingawa ni jambo la kushangilia kwamba Rais Ruto amepata ziara ya kitaifa na atapata ufadhili wa miradi, lakini cha kujiuliza ni kwa ajili ya masilahi ya Kenya zaidi, au Afrika Mashariki zaidi au kwa ajili ya Marekani zaidi?”
Kuhusu Afrika Mashariki
Akizungumzia masilahi ya Afrika Mashariki, Kibamba ametahadharisha nchi wanachama kuchomoka na kwenda kufanya makubaliano na mataifa makubwa bila kushauriana na wenzake.
“Hii tabia ya kuchomoka chomoka peke yako unaweza kusababisha uhasama, inaweza kushusha uaminifu ambao ndio msingi katika uhusiano,” amesema.