Tetemeko ardhi bado lazitesa Uturuki, Syria

Antakya, Uturuki. Tetemeko la ardhi la kipimo cha 6.4 limelikumba jimbo la kusini mwa Uturuki la Hatay na eneo la Aleppo kaskazini mwa Syria usiku wa kuamkia jana Jumanne na kuua watu sita na kuzua hofu mpya baada ya yale ya awali ya Februari 6 na 7.

Kwa jumla matetemeko hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 45,000 katika nchi zote mbili.

Shirika la kukabiliana na majanga la AFAD limeripoti vifo hivyo na kuwa takribani watu 300 wamelazwa hospitalini, huku Syria shirika la misaada la White Helmets likisema takriban watu 150 walijeruhiwa katika eneo la Aleppo.

Kituo cha kunasa majanga hayo Ulaya cha Seismoloji (EMSC) kilisema tetemeko hilo lilipiga kwa kina kidogo cha kilomita 2 (maili 1.2).

Polisi walishika doria huko Antakya huku magari ya kubebea wagonjwa yakikimbilia eneo lililokumbwa na tetemeko karibu na katikati mwa jiji.

Watu wawili walizirai, huku wengine wakijaza mitaa kuzunguka mbuga hiyo ya kati, wakipiga simu za dharura.

Walioshuhudia wameviambia vyombo vya habari kuwa kumekuwa na uharibifu zaidi wa majengo huko Antakya.

Tetemeko la Jumatatu lilipiga mji wa Defne nchini Uturuki saa 2:04 usiku na kishindo chake kilisikika katika mji wa karibu wa Antakya na pia huko Lebanon.

Shirika la udhibiti wa maafa la Uturuki lilisema kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba tetemeko la ukubwa wa 5.8 lilifuatia dakika tatu baadaye na kitovu chake katika Wilaya ya Samandag mkoani Hatay.

Shirika hilo lilirekodi matetemeko mawili zaidi yenye ukubwa wa 5.2 karibu dakika 20 baada ya lile la kwanza Jumatatu.

Picha kutoka kwa shirika la habari la DHA zilionyesha hospitali moja huko Antakya wakiondolewa watu, huku shirika la utangazaji la NTV likiripoti kuwa hospitali moja watu walihamishwa katika jiji la Iskenderun.

DHA ilisema wagonjwa katika chumba cha wagonjwa mahututi walichukuliwa na gari la wagonjwa hadi hospitali za shambani mbali na mjini ili kuendelea na matibabu yao.


‘Dunia inafunguka’

Mwandishi wa habari wa shirika la habari la Ufaransa (AFP) aliripoti matukio ya hofu huko Antakya, huku matetemeko mapya yakiongeza vumbi katika jiji hilo lililoharibiwa vibaya.

Kuta za majengo yaliyoharibiwa zilibomoka huku watu kadhaa, walioonekana kujeruhiwa wakiomba msaada.

Katika barabara moja huko Antakya, Ali Mazlum, 18, aliiambia AFP: “Tulikuwa na AFAD ambao walikuwa wakiitafuta miili ya familia yetu wakati tetemeko lilipopiga.

“Hujui la kufanya. Tukashikana na mara mbele yetu tukaona tena kuta zikianza kuanguka. Tulihisi kama ardhi inafunguka ili kutumeza.”

Mazlum, ambaye ameishi Antakya kwa miaka 12 alikuwa akitafuta miili ya dada yake na familia yake pamoja na shemeji yake na familia yake.


‘Si salama tena’

“Barabara ilisogea kama mawimbi. Jengo lilihamia huku na huko, magari yalisogea kushoto kwenda kulia. Nilipigwa ngwara miguu yangu,” alisema Mehmet Irmak, ambaye anafanya kazi huko Antakya.

“Hatay si mahali salama tena. Tulisikia majengo mengi yakiporomoka ... Tutasubiri siku mpya, lakini sijui nitafanya nini,” aliongeza Irmak, ambaye alikuwa amelala katika gari lake kwa muda wa wiki mbili baada ya tetemeko la kwanza.

Shirika la Madaktari la Syrian American Medical Society (SAMS) limesema hospitali tano inazozisaidia kaskazini-magharibi mwa Syria zilipokea watu kadhaa waliokuwa wamepata majeraha madogo, baadhi yao walipata majeraha hayo wakati kuta za majengo yaliyoharibiwa zilipowaangukia.

Katika maeneo yanayoshikiliwa na Serikali nchini Syria, hospitali za Aleppo pia zilipokea wakazi walioingiwa na hofu, huku watu sita wakijeruhiwa kwa kuangukiwa na kifusi, shirika la habari la Serikali, Sana, lilisema.

Hospitali ya Al Razi huko Aleppo ilipokea majeruhi 47, vyombo vya habari vya Serikali viliripoti.

“Tulitoka nje kwa kasi, hatujui tuliondokaje. Niliogopa kwamba hatima yetu ingekuwa sawasawa na ya wale waliofia chini ya vifusi,” alisema Khadija Al Khalaf, mama mwenye umri wa miaka 45, katika mji wa Azaz.


Hasara kiuchumi

Kwa mujibu wa makadirio ya wataalamu, hasara ya kiuchumi iliyosababishwa na matetemeko hayo inaweza kufikia dola bilioni 4.