Truss kugombea tena ubunge licha ya kujiuzulu kama Waziri Mkuu

Liz Truss

Muktasari:

  • Aliyekuwa waziri mkuu wa Uingereza kwa takribani siku 45, kisha kujiuzulu amesema atasimama tena kama Mbunge kutetea kiti chake cha Norfolk Kusini Magharini.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Liz Truss amesema atagombea tena ubunge kutetea kiti chake katika jimbo la cha Norfolk Kusini Magharibi katika uchaguzi mkuu ujao.


Truss ametangaza kuwania nafasi hiyo ikiwa ni miezi michache tangu ajiuzulu kama Waziri Mkuu wa Uingereza.


Hayo yalithibitishwa jana Desemba 5, 2022 na msemaji wake ikiwa ni mwisho kwa wabunge wa chama tawala cha Conservative kutangaza nia ya kugombea tena katika majimbo yao.


Msemaji huyo amesema: “Nina furaha kuthibitisha kwamba Liz atawania kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu ujao.”


Truss alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Septemba 5, 2022 akichukua nafasi iliyoachwa na Boris Johnson ambaye alijiuzulu katika nafasi hiyo.


Katika kujaza nafasi ya Johnson, Truss aliibuka mshindi dhidi ya Rishi Sunak akipata kura 81,326 huku mgombea mwenzake akipata kura 60,399 katika kinyang’anyiro cha uongozi wa chama cha Conservative.


Baada ya kutwaa wadhifa huo Truss alihudumu katika nafasi hiyo kwa muda wa siku 45 kisha kujiuzulu alhamisi ya Oktoba 20, 2022 akisema kuwa aliingia ofisini wakati wa “machafuko makubwa ya kiuchumi na kimataifa.”


Hiyo ni baada ya bajeti yake ndogo ya kupunguza kodi na kusababisha kuyumba kwa masoko ya fedha ya Uingereza.


Truss anatambulika kama kiongozi na Waziri Mkuu aliyekaa madarakani kwa muda mfupi zaidi katika historia ya Uingereza huku Waziri Mkuu wa pili aliyehudumu kwa muda mfupi zaidi akiwa George Canning ambaye alihudumu kwa siku 119 baada ya kufariki mwaka 1827.


Wakati Truss akipigana, baadhi ya wabunge kutoka chama cha Conservative wameamua kuchukua njia tofauti kwa kujiondoa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kabla ya Januari 2025.


Ijumaa iliyopita, aliyekuwa Waziri wa Afya, Sajid Javid ambaye aligombea nafasi ya Waziri Mkuu mara mbili, alitangaza mipango yake ya kuondoka katika Bunge la nchi hiyo la Westminster.


Javid alisema uamuzi wake wa kutogombea katika uchaguzi wake wa tano ni ule ambao “mepambana nao kwa muda” ambapo amekuwa mbunge wa Conservative wa Bromsgrove tangu mwaka 2010.


Mbunge huyo alichukua nafasi ya Matt Hancock kama Waziri wa Afya baada ya uhusiano wake na Gina Caladangelo kumlazimisha kujiuzulu.


Hata hivyo, aliacha nafasi yake katika Baraza la Mawaziri Julai, kama mtu wa kwanza mwenye jina kubwa na kumtaka Johnson kujiuzulu, na hivyo kusababisha kuanguka kwake saa 48 baadaye