Tshisekedi kumtangaza waziri mkuu wiki hii

Muktasari:

  • Baada ya kushinda urais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) mapema mwaka huu, Felix Tshisekedi amesema kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo atafahamika wiki hii.

Kinsasa, DRC. Rais  wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi amesema kuwa waziri mkuu mpya wa nchi hiyo atafahamika wiki hii.

Tshisekedi alitoa hakikisho hilo jana Jumamosi alipokutana na mabalozi wa Umoja wa Ulaya na wa Canada jijini Kinshasa, kwa mujibu wa RFI.

Hili pia limethibitishwa na msemaji wa Rais Tshisekedi, Kasongo Mwema Yamba Y'amba kupitia ukurasa wake wa twitter, ambaye ameandika kuwa Rais Tshisekledi amewaambia mabalozi hao kuwa, waziri mkuu amepatikana.

Wananchi wa DRC wanasubiri kuona nani atakuwa waziri mkuu kwa sababu kwa mujibu wa katiba, anastahili kutokea kwenye chama chenye wabunge wengi na kwa sasa muungano wa kisiasa wa Rais wa zamani Joseph Kabila ndio ulio na wabunge wengi.

Tangu alipoingia madarakani mapema mwaka huu,  Tshisekedi hajafanikiwa kuunda Serikali yake kutokana na chama chake kuwa na wabunge wa chache.