Ukraine yashukuru mataifa 50 kuwapa msaada

Muktasari:

  • Ukraine imetoa shukrani kwa mataifa ambayo yamejitokeza kutoa msaada tangu kuanza kwa uvamizi wa Urusi nchini humo huku ikiomba msaada zaidi kwa washirika wake kutoka Magharibi.

Dar es Salaam. Ukraine kupitia kwa mawaziri wake wa Mambo ya Nje, Dmytro Kuleba na Waziri wa Ulinzi, Oleksii Reznikov, leo imetoa shukrani zake kuyashukuru mataifa 50 ambayo yalitojilea kuwapa misaada tangu nchi hiyo ilipovamiwa na Urusi mwanzoni mwa mwaka jana.

 Wakieleza uhitaji walionao, Waziri Kuleba na Reznikov, walisema moja ya mahitaji muhimu katika kupambana na uvamizi wa Urusi ulioanza karibu mwaka mmoja uliopita ni kuipatia Ukraine magari ya kisasa ya kivita na kuwapa wanajeshi wa Ukraine uwezo bora wa kutumia vifaa hivyo.
Katika kauli ya pamoja, Kuleba na Oleksii waliiomba Uingereza kutuma vifaru vyake vya Challenger 2 nchini Ukraine, huku wakizitaka nchi ambazo zina mizinga ya Ujerumani ya Leopard 2 kuvipatia ili kusaidia vyema vikosi vya Ukraine huku wakiahidi kutumia vifaa hivyo ipasavyo.
"Tunaahidi kwamba tutatumia silaha hizi na kuwajibika kikamilifu kwa madhumuni ya kulinda eneo la Ukraine ndani ya mipaka inayotambulika kimataifa," mawaziri hao walisema.
Kauli hiyo ya Ukraine imetolewa baada Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin kutembelea Ujerumani kwa ajili ya kukutana na waziri mpya wa Ulinzi wa Ujerumani,  Boris Pistorius kwa ajili ya kufanya mkutano kujadili mahitaji ya kiulinzi ya Ukraine.

Marekani inatarajiwa kutangaza msaada wa jumla ya zaidi ya dola bilioni 2 ambao unajumuisha magari ya kivita ya Stryker.
Waziri Msaidizi wa Ulinzi wa Sera, Colin Kahl aliwaambia waandishi wa habari jana Jumatano kwamba Ukraine inahitaji vifaa vya kuisaidia kurejesha maeneo ambayo yamevamiwa na Urusi.
Alisema mizinga ya Abrams haitakuwa msaada bora kutoa kwa wakati huu, akiashiria changamoto zilizopo katika kuzitumia na kuzitunza.
Tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine mwezi Februari mwaka jana, watu zaidi ya 42,000 wanakadiriwa kupoteza maisha, 54,000 wamejeruhiwa, 15,000 hawajulikani walipo na zaidi ya watu milioni 14 wameachwa bila makazi.


 Mwisho