Unicef: Watoto milioni 67 duniani hawakupata chanjo miaka 3
Muktasari:
- Ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, imesema watoto milioni 67 hawakupata chanjo moja au zaidi wakati wa janga la Uviko-19 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupungua kwa imani ya chanjo.
Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto (Unicef), limesema watoto milioni 67 duniani kote hawakupata chanjo za kuzuia magonjwa kutokana na uhaba wa rasilimali, migogoro, kupungua kwa imani ya chanjo na kukatishwa kwa huduma iliyotokana na mifumo duni ya afya.
Utafiti uliofanywa na mradi wa ‘The Vaccine Confidence Project’ na kutolewa leo na Unicef imesema mtazamo wa umma juu ya umuhimu wa chanjo ulipungua katika nchi 52 kati ya 55 zilizofanyiwa utafiti kwanzia 2019 hadi 2021.
Baada ya kuanza kwa janga la Uviko-19, ripoti inasema mtazamo wa umuhimu wa chanjo kwa watoto ulipungua zaidi ya theluthi moja katika nchi za Jamhuri ya Korea, Papua New Guinea, Ghana, Senegal na Japan.
Hata hivyo ripoti hiyo inazitaja nchi za China, India na Mexico kuwa ndizo zilizoonyesha mtazamo imara wa umuhimu wa chanjo kwa watoto.
Inaelezwa katika nchi nyingi, watu walio na umri wa chini ya miaka 35 na wanawake walikuwa na imani ndogo dhidi ya chanjo kwa watoto baada ya janga la Uviko-19 kuanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Unicef, Catherine Russell, amesema kipindi cha Uviko-19, wanasayansi walitengeneza chanjo haraka ambazo ziliokoa maisha mengi, lakini licha ya mafanikio haya ya kihistoria, hofu na taarifa potofu kuhusu aina zote za chanjo zilienea kwa upana kama vile virusi vyenyewe.
"Ripoti hii ni ishara ya onyo inayotia wasiwasi. Hatuwezi kuruhusu imani katika chanjo za kawaida kuwa mwathirika mwingine wa janga hili.
“Vinginevyo, wimbi linalofuata la vifo linaweza kuwa la watoto wengi walio na surua, diphtheria au magonjwa mengine yanayoweza kuzuilika,” amesema Russell kwenye ripoti hiyo.
Amesema kupungua kwa imani kulichochewa na janga la Uviko-19 lililokatiza chanjo ya watoto karibu kila mahali duniani.
Ili kukabiliana na janga hili la maisha ya watoto, Unicef imetoa wito kwa Serikali kuunga mkono dhamira yao ya kuongeza ufadhili wa chanjo za watoto ili kuzuia milipuko ya magonjwa.